Matamasha yawakumbusha mbali | Mwanaspoti

WAKATI leo likifanyika Tamasha la Simba Day, likifuatiwa na Wiki ya Mwananchi keshokutwa Ijumaa, wachezaji waliowahi kucheza Simba na Yanga wametoa kumbukumbu zao juu ya matamasha hayo.

Simba Day inayofanyika leo, ni msimu wa 17 tangu Klabu ya Simba kulianzisha mwaka 2009, huku upande wa Yanga ikifanya Wiki ya Mwananchi kwa mwaka wa saba.

Katika matamasha hayo, mbali na burudani mbalimbali na utambulisho wa kikosi cha msimu wa 2025-2026, pia kutakuwa na mchezo wa kirafiki, Simba ikikabiliana na Gor Mahia na Yanga dhidi ya Bandari zote za Kenya.

Aliyekuwa beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye amejiunga na Transit Camp inayoshiriki Ligi ya Championship, alisema: “Wiki ya Mwananchi imeniachia kujua kazi yangu ina thamani kubwa kutokana na mashabiki kujaa uwanjani kuja kutusapoti, siyo kwamba hawana kazi za kufanya, hilo linaongeza nguvu kwa mchezaji kuongeza bidii ya mazoezi kuhakikisha anawapa furaha ya kujitolea muda wao.”

Kwa upande wa kiungo wa zamani wa Yanga ambaye ametua Mbuni FC ya Ligi ya Championship, Said Juma Makapu, alisema: “Ni tamasha lililotutambulisha wachezaji na kuongeza thamani ya kazi yetu, ukiona watu wanasafiri kutoka ndani na nje ya nchi, ina maana wanathamini mnachokifanya.”

Kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Abdulaziz Makame anayeitumikia Tabora United, alisema: “Kupitia matamasha ya klabu hizo yalinifunza namna kazi yangu inavyopendwa na watu ambao wanasafiri kutoka pande mbalimbali za dunia na kujumuika pamoja, pia limeniachia kumbukumbu ya upendo.”

Winga wa zamani wa Simba na Yanga, Yusuph Mhilu anayecheza Geita Gold ya Championship alisema: “Niliondoka Yanga 2018, Wiki ya Mwananchi ilianzishwa 2019 nikiwa Ndanda, mimi nilikuwa sehemu ya Simba Day 2021/22 nilipojiunga nao nikitokea Kagera Sugar.

“Tamasha hilo limeacha kumbukumbu ya kuona kazi yangu ina thamani kubwa, kutokana na mashabiki kuja kujumuika pamoja kutoka ndani na nje ya nchi.”