Matumizi ya AI kwenye matibabu yawaibua wataalamu wa afya

Dar es Salaam. Matumizi chanya ya teknolojia ya Akili Unde (AI) katika utambuzi wa magonjwa na urahisishaji wa matibabu yameelezwa kuwa miongoni mwa afua muhimu zinazoweza kubadilisha taswira ya sekta ya afya barani Afrika.

Kauli hiyo imetolewa na wataalamu wa afya waliohudhuria ufunguzi wa Maonesho ya 26 ya Africa 2025 MEDEXPO, yanayofanyika kuanzia leo, Septemba 10 hadi 12, 2025, jijini Dar es Salaam, yakihusisha zaidi ya nchi 25 kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.

Wataalamu hao wameeleza kuwa, mbali na AI, maendeleo katika uzalishaji wa vifaa tiba vya kisasa vinavyoendana na mahitaji ya wahudumu na wagonjwa, pamoja na upatikanaji wa matibabu sahihi na thabiti, ni hatua muhimu katika kuinua huduma za afya.


Katika maonesho hayo ya kimataifa yanayowakutanisha watengenezaji, wasambazaji na wauzaji wa vifaa tiba, washiriki wanabadilishana ujuzi na uzoefu kuhusu namna bora ya kutumia teknolojia mpya katika kutoa huduma bora za afya.

Akili Unde ni teknolojia inayowezesha mashine na kompyuta kuiga uwezo wa binadamu, ikiwemo kujifunza, kufanya uamuzi, kubuni na kutatua changamoto. Mbali na sekta ya afya, teknolojia hiyo inazidi kuenea katika nyanja za elimu, fedha, mawasiliano na nyinginezo.

Wataalamu wamehimiza wabunifu na wadau wa teknolojia kuendelea kuwekeza katika suluhisho za AI ili kurahisisha huduma kwa wagonjwa, kuongeza ufanisi wa watumishi wa afya, pamoja na kupunguza muda wa kutoa huduma.

Akizungumza baada ya kuzindua maonesho hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Dk Mpoki Ulisubisya, amesema hitaji kubwa linalohitajika kwa sasa ni urahisishaji wa huduma za matibabu.


“Tunahitaji afua ya vifaa vitakavyosaidia kupunguza muda kutoka mgonjwa anapokuja kwenye kituo hadi anapopata matibabu. Mfano, ikitokea tumepata Akili Unde inayosaidia kufahamu mgonjwa anashida gani na apewe tiba gani kwa kuangalia tu, itakua imepunguza muda wa kupanga foleni.

“Aidha, itokee mashine itakayogundua mtu mwenye shida ya nyonga kwa kumuangalia tu anavyotembea kisha ikasema apandikizwe nini, itakua imesaidia, au tupate mashine itakayogundua magonjwa yote kwa damu tu, itasaidia kupunguza muda na kugundua ugonjwa mapema,” amesema.

Maneno ya Dk Ulisubisya yanarandana na ya Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, aliyesema matumizi ya dijitali katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba yana nafasi kubwa.

“Akili Unde inapaswa kuwa katika uzalishaji na watumiaji, ndio maana tunakutana kujadili na watafiti na wavumbuzi kuwapa mawazo yetu ya kitaalamu ili wakaboreshe kwa ajili ya kutoa huduma bora, salama, kwa vifaa rafiki vinavyowafaa Watanzania,” amesema.


Aidha, amesema viwanda vinaweza kuja Tanzania kuwekeza ili kuzalisha dawa hapa nchini kwa kuwa kuna watumiaji wengi.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Expo Group, Duncan Njage, amesema maonesho hayo ni fursa katika suala zima la ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa afya.