Miaka 10 iliyopita, Taifa lilipokuwa linauelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, aliibuka na kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” iliyobeba tafsiri ya maono yake ya kuwafanya Watanzania wafanye kazi bila lelemama.
Mwaka 2020, mgombea urais wa Chama cha The United People’s Democratic Party(UPDP), Twalib Ibrahim Kadege, alijinadi kwa kaulimbiu ya “Kazi Mperampera.”
Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, utakaofanyika Oktoba 29, UPDP wameendelea kumwamini Kadege, ambaye safari hii ameboresha kaulimbiu yake, anasema: “Spidi Mperampera hadi Ikulu.”

Kwa ukamilifu, kaulimbiu hiyo inatamkwa: “Spidi Mperampera hadi Ikulu, Amani na Utulivu ni Ngao Yetu.”
Ni kaulimbiu ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia UPDP, Twalib Ibrahim Kadege, ambaye anasema anataka Watanzania wamwamini, wampe ridhaa ya kuwaongoza, kisha awapeleke “mperampera.”
Kadege anasema pamoja na kuja na kaulimbiu inayoitangulia mbele ile ya Dk Magufuli mwaka 2015, lakini anamheshimu mno kwa jinsi alivyoihudumia nchi katika uongozi wake akiwa Rais.
Anakiri kuwa Dk Magufuli alikuwa Rais wa mfano, aliyeweza kuipa heshima nchi kwenye uso wa kimataifa. Pia, anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi bora na makini.
Alikuwepo baba, jina lake Ibrahim Hamis Kadege na mama, Zalia Mohammed Kikombe. Februari 14, 1952, siku ambayo walimwengu wenye mahaba yao husherehekea siku inayoitwa “Valentine’s Day” ndipo walipata mtoto wa kiume, wakamwita Twalib. Kwa unyoofu, huyo ndiye Twalib Ibrahim Kadege.
Na huyo Twalib ndiye akawa kitinda mimba, kwa maana, baada ya kuzaliwa yeye, hakuongezeka mwingine, si kwa baba wala mama yake. Kwa kifupi, Twalib Kadege ni mtoto wa mwisho kati ya sita wa Ibrahim Kadege na Zalia Kikombe.

Kijiji cha Kiwawa Kingongo, kilichopo Kilwa Masoko, mkoani Lindi, ndiyo maskani ya kujidai ya Twalib Kadege. Alizaliwa hapo na alikulia kijijini hapo. Mwaka 1963, akiwa na umri wa miaka 11, Kadege alianza darasa la kwanza, Shule ya Msingi Lihimalyao, iliyopo Tarafa ya Pande, wilayani Kilwa, Lindi.
Mwaka 1964, alihitimu darasa la nne. Kadege, alifaulu mtihani wa darasa la nne, hivyo mwaka 1965, alichaguliwa kuendelea na darasa la tano katika Shule ya Msingi Msanga, wakati huo ikitambulika kama middle school, iliyopo Kilwa Masoko.
Alisoma hapo mpaka darasa la sita mwaka 1966, kabla ya kuhamia Shule ya Msingi Pande-Extended, alikomalizia darasa la sita na kuhitimu la saba mwaka 1967.
Mwaka 1970, Kadege aliajiriwa na Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, Ubungo, Dar es Salaam, kama mwendeshaji wa mitambo.
Baada ya miaka 14 ya kufanya kazi katika sekta tofauti za uzalishaji wa nguo kiwandani, ilipofika mwaka 1984, alipewa nafasi na uongozi wa kiwanda kuendelea na masomo ya juu.
Uongozi wa Kiwanda cha Urafiki ulianzisha utaratibu wa kuwaendeleza kielimu wafanyakazi wake, hivyo wakateua baadhi ya vyumba kiwandani na kuvifanya madarasa, kisha wakawa wanawaalika walimu kutoka shule na vyuo mbalimbali ili kwenda kufundisha wafanyakazi palepale kiwandani.
Ni kupitia utaratibu huo, Kadege alipata nafasi ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka 1980. Mwaka 1982 alifanya mitihani ya kidato cha pili na kupata namba, ambayo ilimuwezesha kufanya mtihani wa kidato cha nne kama mtahiniwa binafsi mwaka 1988.
Kadege anaeleza mtihani wa kidato cha nne mwaka 1988, alifanya masomo matatu. Kiingereza alipata ufaulu wa daraja C, Kiswahili (B) na Siasa (D).
Ufaulu huo wa kidato cha nne ulimwezesha kusoma faini ya teknolojia ya utengenezaji wa nguo.
Mwaka 1989, Kadege alipewa fursa nyingine ya kusoma. Safari hiyo alisoma astashahada ya teknolojia ya utengenezaji nguo (textile technology). Kama kawaida, masomo hayo alisomea palepale Urafiki, walimu walikuwa wakialikwa kwenda kiwandani kufundisha. Alihitimu na kukabidhiwa cheti daraja la tatu kama mtaalamu wa utengenezaji nguo.

Mgombea urais wa chama cha UPDP, Twalib Kadege akiwasalimia wakazi wa Igoma wakati wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu zilizofanyika Igoma jijini Mwanza.
Mwaka 1998, Kadege alianza masomo ya sekondari ya juu. Akiwa amemaliza kidato cha tano, akielekea kuanza masomo ya kidato cha sita, Kiwanda cha Urafiki kilibinafsishwa. Ubinafsishwaji huo ulisababisha mabadiliko makubwa ya uendeshaji.
Uongozi mpya ulioingia kiwandani baada ya ubinafsishaji, haukukubali utaratibu uliokuwapo wa kuwaendeleza kielimu wafanyakazi wake, kwa hiyo Kadege hakuweza kukamilisha masomo ya kidato cha sita na hakufanya mitihani.
Kadege anasema wakati Kiwanda cha Urafiki kinabinafsishwa, alikuwa pia anasoma Uandishi wa Habari, ngazi ya astashahada, lakini hakuendelea kukamilisha masomo, kwani alikuwa akisomea palepale kiwandani kwa utaratibu uliokuwapo.
Mwaka 1999, Kadege aliacha kazi Urafiki, kwa kile anachoeleza hakuwa na maelewano na uongozi mpya. Anasema hiyo haikumhusu yeye peke yake, bali wafanyakazi wengine wengi. Kwa mazingira hayo, kwa moyo mweupe, aliacha kazi.
Kadege alipoondoka Urafiki, alianza kujishughjulisha na kilimo, vilevile kuweka mkazo zaidi katika siasa.
Ni mkulima mwenye mashamba ya mpunga na ufuta, Rufiji, mkoani Pwani, pia Turiani, Morogoro, pamoja na Lutando, Mkuranga, mkoani Pwani. Ni mkulima wa minazi pia.
Kadege ana mashamba ya korosho yaliyopo Nang’oo, Pande, wilayani Kilwa, mkoani Lindi. Kwa sifa hiyo, Kadege anaridhika endapo utamtambulisha kama mtaalamu wa teknolojia ya uzalishaji nguo ambaye amegeukia kilimo, lakini pia mwanasiasa.
Kadege yupo kwenye siasa kwa miaka 33 sasa. Mwaka 1992, alikuwa mjumbe wa tawi la CCM, Kiwanda cha Urafiki, Ubungo, Dar es Salaam. Mwaka 1995, upepo wa siasa za mageuzi uliochangiwa na aliyekuwa mgombea urais wa NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema, ulimzoa, ukamtoa CCM na kumtua NCCR-Mageuzi.
Mwaka 1995, alichaguliwa kuwa Katibu wa NCCR-Mageuzi, tawi la Ubungo (Urafiki na National Housing). Mwaka 1996, alichaguliwa kuwa Katibu wa NCCR-Mageuzi Kata ya Ubungo, Dar es Salaam.
Mwaka 1999, baada ya mgogoro wa uongozi NCCR-Mageuzi uliotokana na mivutano ya viongozi, makundi mawili, la Mrema (Mwenyekiti) na Katibu Mkuu, Mabere Marando, chama kiligawanyika makundi mawili.
Mrema alipohama NCCR-Mageuzi na kwenda TLP, alisababisha wengi wamfuate, Kadege akiwa miongoni mwao.
Alihamia TLP mwaka 1999 alikochaguliwa kuwa katibu wa chama hicho Kata ya Ubungo. Mwaka 2000, Kadege akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TLP Jimbo la Ubungo. Mwanzoni mwa mwaka 2006 alihama TLP akajiunga na UPDP.
Alibaki kuwa mwanachama wa kawaida wa UPDP mpaka mwaka 2010, alipochaguliwa kuwa mjumbe wa Halmshauri Kuu ya Taifa ya UPDP. Mwaka 2010 aligombea udiwani Kata ya Manzese, Ubungo, Dar es Salaam, lakini hakushinda.
Mwaka 2015, alikuwa mmoja wa wanachama wa UPDP walioteuliwa na Kamati Kuu ya chama hicho, kuwa wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi.
Kwa kuwa mjumbe wa kamati hiyo, alikosa sifa ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi. Hata hivyo, baada ya uchaguzi, aliyeshinda uenyekiti, Fahmi Nassoro Dovutwa, alimteua kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.
Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Kadege aliteuliwa kuwa meneja kampeni za mgombea urais wa UPDP, Dovutwa.
Agosti 9, 2018, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa UPDP Tanzania Bara, Felix Makua, alihamia Ada-Tadea. Kadege akateuliwa kuwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UPDP (Tanzania Bara).
Desemba mosi, 2019, Dovutwa, alifutwa uanachama wa UPDP, hivyo kupoteza sifa ya kuwa mwenyekiti. Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa UPDP Zanzibar, Abdallah Mohamed Hamis, akawa Kaimu Mwenyekiti.
Siku hiyohiyo, Hamis alimteua Kadege kuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara) na kuthibitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa UPDP.
Julai 29, mwaka 2020, katika ukumbi wa Equator Grill, wilayani Temeke, Dar es Salaam, UPDP walifanya mkutano mkuu kuchagua viongozi, Kadege aligombea na kushinda uenyekiti wa chama hicho.
Sophia Kawambwa, ndiye mke wa Kadege, ana watoto watano walio hai ambao ni Hamis, Rehema, Zamda, Rahim na Neema. Mtoto wa sita wa Kadege ni Salum, ambaye Mungu alishamchukua.
Kadege anataja vipaumbele vyake katika mbio zake za urais 2025 kuwa ni kilimo, akisema ardhi kwanza, kilimo ni kiwanda mama.
Kadege anaahidi matibabu bure kwa wote. Kuhusu elimu, anasema atabadili mfumo ili ya sekondari iwe ya kuwapa ujuzi wanafunzi.
Anasema ilani ya UPDP 2025 haijaacha kitu. Anaahidi endapo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wazee kila mmoja atakuwa analipwa Sh500,000 kwa mwezi.