Geita. Mgombea urais wa Chama cha United Democratic Party (UDP), Saumu Rashid amesema chama chake kimejipanga kutatua changamoto kubwa zinazowakabili Watanzania kwa kuhakikisha upatikanaji wa majisafi na salama, elimu bure hadi chuo kikuu, huduma za afya nafuu na uwekezaji wenye tija katika rasilimali za Taifa.
Akizungumza leo Septemba 10, 2025 kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Nyankumb Manispaa ya Geita, Rashid amesema wananchi wa mkoa huo wamesahaulika licha ya kuwa na rasilimali nyingi, ikiwamo madini na maji ya Ziwa Victoria.
“Haiwezekani wananchi wa Geita wawe jirani na Ziwa Victoria, lakini bado wanahangaika na tatizo la maji. Serikali ya UDP itaweka mpango wa uchimbaji wa visima virefu, uvunaji maji ya mvua na kuvuta maji ya ziwa ili kuhakikisha kila kaya inapata maji safi na salama. Lengo letu ni kumtua mama ndoo kichwani,” amesema.
Akigusia sekta ya elimu, Rashid amesema UDP imedhamiria kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu na kuondoa michango inayowalemaza wazazi.
“Tunataka elimu yenye tija, itakayowapa vijana ujuzi na Taifa wataalamu wa kutosha kwa maendeleo ya kiuchumi,” amesema.
Katika sekta ya afya, ameahidi uwekezaji mkubwa kwenye huduma za msingi, ikiwa ni pamoja na kuweka bima ya bei nafuu kwa wananchi wote na kuhakikisha watoto chini ya miaka mitano wanapata huduma bora bila vikwazo.
Amesema chama chake kimelenga pia kuinua wanawake kiuchumi kwa kuhakikisha mikopo inayotolewa na halmashauri wanaipata bila vikwazo, lakini pia watahakikisha wanashiriki moja kwa moja kwenye miradi ya madini.
Aidha, chama hicho pia kitahakikisha wachimbaji wadogo wanapewa vifaa na maeneo ya kuchimba ili kuwainua kiuchumi.
Ameahidi kila mkoa nchini utakuwa na kiwanda kulingana na rasilimali zilizopo ili kuongeza ajira kwa vijana na kukuza uchumi.
“Tukiwa na viwanda vya kuchakata bidhaa zetu ndani ya nchi, tutakuwa na ajira nyingi na kipato kwa wananchi tunaomba Oktoba 29 mtuchague sisi UDP ili tulete maendeleo,” amesema.
Kwa upande wa kilimo, amesema UDP itahakikisha wakulima wanapatiwa ruzuku ya kutosha na masoko ya mazao ya biashara ili kuongeza kipato na chakula cha kutosha.
Pia, ameahidi mikopo nafuu kwa wajasiriamali na kuondoa upendeleo unaofanyika katika mikopo ya halmashauri.
Kuhusu vita dhidi ya rushwa, Rashid amesema Serikali ya UDP itaweka mikakati madhubuti kuhakikisha wananchi wanapata huduma bila kikwazo, huku akisisitiza Tanzania bila rushwa inawezekana.
Mgombea mwenza wa urais wa UDP, Juma Hamis Faki amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani na utulivu, akisisitiza kuwa uchaguzi siyo vita bali ni demokrasia.
“Nawaomba sana wananchi hii ni nafasi ya kumchagua kiongozi unayemtaka, tupige kura kwa utulivu kisha turudi nyumbani tukisubiri matokeo ya tume, uchaguzi sio vita ni demokrasia,” amesema.
Mgombea ubunge Jimbo la Nyang’hwale kupitia UDP, Malendeja Patrick amesema akishinda katika uchaguzi ujao atapigania miradi ya maji, ujenzi wa barabara ya lami kutoka Geita kwenda Nyang’hwale na kutetea wachimbaji wadogo wanaonyang’anywa maeneo ya uchimbaji.
Katika mkutano huo mgombea urais huyo pia amezindua tawi la UDP, Kata ya Nyankumbu.