:::::::::
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Dellilah Kimambo amesema kuwa jamii inatakiwa kubadili mitazamo juu ya jambo la kujiua na kuamsha dhamira ya pamoja ya kuokoa maisha, kupunguza unyanyapaa ili Kujenga mustakabali wa kizazi kinachojali afya ya akili.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Kuzuia Kujiua Duniani leo Septemba 10, 2025 Jijini Dar es saalam, Dkt. Kimambo amesema kuwa tatizo kubwa husababishwa na ukimya na unyanyapaa ambao upo kwenye familia au jamii zinazotuzunguka.
“Hapa Tanzania, kama ilivyo duniani kote, tatizo hili mara nyingi hufunikwa na ukimya, unyanyapaa na kutoelewa. Lakini nyuma ya kila takwimu kuna hadithi ya kibinadamu: ni mama, baba, kaka, dada, mwanafunzi au jirani aliyepoteza matumaini au simulizi za maumivu au upweke,” amesema Dkt. Kimambo.
Aidha Dkt. Kimambo ameongeza kuwa MNH kupitia Idara ya Afya na Magonjwa ya Akili inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kimatibabu kwa manusura wa vitendo vya kujiua na familia zao ikiwemo ushauri nasaha, tiba ya magonjwa ya akili, elimu kwa jamii kupitia mikutano, semina, warsha na mahojiano kupitia vyombo vya habari.
Maadhimisho ya Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani huadhimishwa Septemba 10 kila mwaka ambapo kwa mwaka 2025 kaulimbiu inasema “badili mtazamo juu ya matukio ya kujiua” huku Takwimu za dunia zinaonesha kuwa zaidi ya watu 720,000 hufariki kila mwaka kwa kujiua ikikadiriwa mtu mmoja hupotea kila baada ya sekunde 40 na asilimia 90 ya vitendo vya kujiua vinatokana na magonjwa ya afya ya akili.