NENO KWA NENO UJUMBE MZITO WA DK.BASHIRU KWA WATANZANIA KUHUSU RAIS SAMIA

“Niwape ushuhuda wa pili kiongozi wetu huyu alionesha umakini, utulivu na ujasiri mpaka tukavuka”

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

KWA mara ya kwanza Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Cha Mapinduzi(CCM) na Katibu Mkuu Kiongozi Dk.Bashiru Ally amevunja ukimya kwa kutoa ya moyoni baada ya kuwa kimya kwa miaka minne bila kupanda katika majukwaani.

Dk.Bashiru ambaye ni Mratibu wa Kampeni za mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ametumia nafasi hiyo kutoa ya moyoni lakini kutoa sababu za msingi na maalum Watanzania kumchagua Dk.Samia katika uchaguzi mkuu mwaka huu ili aendelee kuwa kiongozi wetu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Bombadia mkoani Singida ,Dk.Bashiru mbele ya Dk.Samia na maelfu ya wananchi wa Mkoa huo alianza kwa kueleza :”Ndugu  mwenyekiti sipendi kuweka chumvi kwa yale yaliyosemwa na wagombea. 

“Nikawaida mimi kama mratibu kufafanua mambo ambayo yana mantiki kwa chama chetu na ndiyo msingi wa kifalsafa na kiitikaji wa chama chetu ambacho sasa hivi kinaomba ridhaa kuendelea kuongoza taifa letu, mdogo wangu Jesca Kishoa mgombea wa Iramba Mashariki amegusia kidogo

“Jambo  ambalo analiona kama sifa muhimu na maalum ya uongozi wako (Rais Samia)na sifa hiyo kama alivyosema kwa usahihi inatosha pia kuwashawishi watanzania kukupa ridhaa kwa mara ya pili uwe kiongozi wetu.”

Akiendelea kueleza Dk.Bashiru amesema  tofauti ya Jesca Kishoa na yeye kuhusu sifa hiyo ni kwamba Kishoa alikuwa nje akifuatilia mimi (yeye)alikuwa katikati ya jambo hilo na huwa hapendi kusema suala hilo kwa sababu kila akıjaribu hushindwa kudhibiti hisia zake.

“Kwasababu  ni hali ambayo sikuwahi kuhitarajia katika maisha yangu. Kishoa amezungumza kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi uliyoikuta wakati unapewa jukumu la kuongoza taifa letu, watanzania ni mshahidi kwamba tulivuka kutoka ugonjwa mpya kabisa wa Covid bila kuathirika sana kiuchumi ukilinganisha na nchi nyingine.

“Na watanzania ni mashuhuda kwamba uliwavusha kwa tukio ambalo si la kawaida kutokana na tukio lisilo la kawaida ambalo halijawahi kutokea katika nchi yetu na hata katika ukanda wa Afrika Mashariki kumpoteza kiongozi kipenzi cha wananchi baada ya kupewa kura nyingi baada ya Uchaguzi.

“Hao wanaoshuhudia na nimewasikia wengi akiwemo mzee Kikwete (Jakaya Kikwete) walikuwa nje kama watazamaji.Mimi nilikuwa katikati ya vikao vinavyoshughulikia jambo hilo.

“Kwahiyo niwape ushuhuda msiwe na shaka Watanzania wenzangu huyu kiongozi wetu ana utulivu wa aina yake, ana ujasiri na umakini wa aina yake kwasababu hali hiyo ilihitaji utulivu , ilihitaji umakini , ilihitaji ujasiri na nakubaliana na Jesca Kishoa sifa hiyo pekee inatosha kumuombea nafasi atuongoze.

“Maeneo mengine matukio hayo mawili yakitokea katika nchi ambazo zinazojijenga zinaacha maafa makubwa, mataifa husambaratika .Leo taifa letu sio tu linaamani lakini ni taifa moja.”

Akiendelea kueleza Dk.Bashiru amesema yeye  ni mtafiti anadhani msingi wa sifa hizo zimetokana na uwezo wa Chama Cha Mapinduzi kuwaandaa viongozi.

“Na kwahiyo sio sifa zake ni sifa za Chama chake kilichomuibua,kilichomlea na kumpa misimamo na yeye akaisimamia.Kwahiyo huyu sio mgombea bora wa urais, ni mgombea bora wa urais wa Chama bora 

“Jambo la pili la kifalsa na kiitikadi kwa sera za CCM ni suala la usawa wa kibinadamu na usawa wa binadamu ndugu yangu haimaanishi binadamu wote tutengeneze usawa tuwe na kimo kimoja hapana, haimaanishi kuwa na rangi moja ,jinsia moja hapana.

“Haimaanishi mapato yanayofanana hapana usawa wa kibinadamu kwa mujibu wa itikadi na falsafa ya CCM ni kuheshimu utu wa kila binadamu awe mrefu au mfupi kama mbili.Katika suala la heshima ya utu wake yeye ni sawa.

“Na ndio maana ukisikiliza hiyo habari ya shule,maji ,afya CCM haiwezi kufanya tofauti na kwahiyo Chama Cha Mapinduzi kinajenga shule, zahanati, vutuo vya afya ,maji, mawasiliano na maeneo mengine hili ni kulinda heshima ya utu wa watu wote.”