Morogoro. Baadhi ya watumiaji wa vyombo vya moto, baiskeli na watembea kwa miguu wameng’atwa na nyuki waliokuwa wamevamia eneo la Msamvu Mataa, Manispaa ya Morogoro, huku wengine wakipata majeraha baada ya kudondoka na vyombo vyao vya usafiri wakijaribu kuwakimbia nyuki hao.
Tukio hilo limetokea leo Jumatano Septemba 10 kwenye nguzo za taa za barabarani zilizopo Msamvu, baada ya nyuki hao waliokuwa wameweka makazi eneo hilo kutanda na kuleta madhara huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro likifika na kufanya uokoaji.
Akitoa taarifa baada ya kufanya uokoaji, kaimu kamanda wa jeshi hilo, Shaabani Marugujo amesema taarifa za tukio hilo zilitolewa na msamalia mwema aliyefahamika kwa jina la Rajabu Omary na baada ya taarifa hizo kikosi cha askari kilifika eneo hilo na kukuta nyuki wakiwa wamezagaa angani, kwenye makazi ya watu na vibanda vya biashara vilivyopo jirani na eneo hilo.
Marugujo amesema katika kipindi hiki cha kiangazi kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya uvamizi wa nyuki kwenye maeneo mbalimbali, lakini wamekuwa wakifanya uokozi wa haraka kabla ya kutokea kwa madhara makubwa.
Kiongozi wa timu ya uokozi wa tukio hilo kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji S/SGT, Alexander Makuluni amesema baada ya kukagua eneo la tukio alibaini nyuki hao wameweka makazi kwenye moja ya taa za barabarani.
Makuruni amesema kutokana utaalamu walionao waliweza kuwatuliza nyuki hao na kurejesha hali usalama katika eneo hilo na sasa barabara hiyo imefunguliwa na inatumika kama kawaida.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Rajabu Hassan amesema nyuki hao walikuwepo katika nguzo ya taa za barabarani kwa muda mrefu lakini hawakuwahi kuleta madhara kama ya leo.
Hassan amesema akiwa kwenye kijiwe chake cha bodaboda, ghafla aliona watu wakikimbia na wengine kuanguka na bodaboda zao baada ya nyuki hao kuzagaa katika eneo hilo.
“Tunashukuru Mungu waokoaji kutoka Jeshi la Zimamoto wamefika kwa haraka na kuwatuliza, vinginevyo madhara yangekuwa makubwa maana watu walishataharuki na wengine walikuwa wakikimbia hovyo barabarani, hawa nyuki muda mrefu wameweka makazi kwenye nguzo ya taa za barabarani lakini nadhani leo watakuwa wamechokozwa,” amesema Hassan.