RAIS SAMIA APONGEZWA KWA KUTOA AJIRA MALIASILI NA UTALII

…………….

Na Sixmund Begashe, Mwanza

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kutoa fursa ya ajira kwa vijana waliohitimu vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Uhifadhi) wa Wizara hiyo, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, katika mahafali ya 61 ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi (PWTI), yaliyofanyika jijini Mwanza mwishoni mwa wiki.

CP Wakulyamba amesema chuo hicho kimeendelea kuwa chachu ya mafanikio ya uhifadhi nchini kwa kutoa wataalamu mahiri wa wanyamapori, mazingira na utalii, jambo linaloiwezesha serikali kutoa kipaumbele katika ajira.

 “Pamoja na serikali kuwa mwajiri mkuu, bado ni changamoto kutosheleza mahitaji ya soko la ajira. Natoa rai kwa sekta binafsi inayojihusisha na uhifadhi wa misitu, wanyamapori na biashara zinazohusiana na utalii, kutoa nafasi kwa vijana hawa ili kuongeza tija na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira,” amesema.

Vilevile, amewataka wahitimu kutumia ujuzi walioupata kwa maslahi ya Taifa.

Naye, Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo wa wizara hiyo, Dkt. Edward Kohi, alisema wizara itaendelea kufanya tafiti ili kubaini hali ya ajira kwa wahitimu wa vyuo vyote vinavyosimamiwa na Maliasili.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya PWTI, Prof. Agnes Sirima, ameahidi kuendeleza ushirikiano na wizara katika kuinua uwezo wa taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa chuo hicho, kozi ndefu zilianza Oktoba 3, 2024, zikihusisha wanachuo 446 wa mwaka wa masomo 2024/25, ambapo wanawake walikuwa 124 (sawa na asilimia 27.64) na wanaume 322 (sawa na asilimia 72.36) na wahitimu waliofanikiwa kuhitimu mwaka huu ni 313.