Sababu Lissu kuomba muda zaidi, Mahakama yatoa kauli

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu ameiomba Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, impe muda apitie uamuzi wa kesi zilizowasilishwa na upande wa mashtaka walipojibu hoja za pingamizi lake alizowasilisha katika kesi ya jinai inayomkabili.

‎Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume cha kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutamka maneno kuhusu kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025.

Kesi inasikilizwa na majaji watatu, jopo likiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, James Karayemaha kutoka Mahakama Kuu Songea na Ferdinand Kiwonde wa Mahakama Kuu Bukoba.

Lissu aliweka pingamizi akipinga Mahakama kuendelea na usikilizaji wa kesi akidai ni batili kutokana na kasoro za kisheria katika mwenendo wa hatua za awali.

Kutokana na pingamizi hilo mahakama ilisimamisha usikilizwaji wa shauri hilo ili kushughulikia kwanza pingamizi la Lissu aliyewasilisha hoja zake Septemba 8 na jana (Septemba 9) kisha upande wa Jamhuri kupitia jopo likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga lilianza kuzijibu na kuhitimisha leo Septemba 10, 2025.

Mawakili wa Jamhuri mbali na kurejea vifungu vya sheria pia, walirejea kesi zilizoamuliwa na Mahakama ya Rufaa kuhusu hoja zilizobishaniwa.

Baada ya Jamhuri kuhitimisha hoja, Lissu alizijibu na baada ya takribani saa mbili aliomba ahirisho ili apate muda wa kupitia uamuzi wa kesi zilizorejewa na kuwasilishwa mahakamani na Jamhuri.

“…kama itawapendeza naomba mnipe maelekezo ili niweze kupata nafasi ya kupitia kesi zilizoamuliwa na Mahakama ya Rufaa ambazo wenzangu upande wa mashtaka walizitumia kama rejea wakati wakijibu hoja na kesho nije nijibu hoja zilizotolewa na upande wa mashtaka,” ameomba Lissu.

Jaji Ndunguru aliuliza upande wa mashtaka kama una pingamizi juu ya ombi hilo. Wakili Katuga amesema kwa kuwa wanataka haki katika usikilizwaji, hawana pingamizi.

“Sisi hatuna pingamizi juu ya ombi hilo, labda Mahakama itoe maelekezo mengine,” amesema Katuga.

Jaji Nduguru alikubali ombi la Lissu na kuahirisha kesi hadi Septemba 11, 2025, atakapoendelea kujibu hoja za upande wa Jamhuri.

Awali, akijibu hoja za Lissu, Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema alidai: “Mshtakiwa alishauriwa kama anataka kuleta mashahidi ambao anadai hawakuorodheshwa katika orodha ya mashahidi, anatakiwa kwenda kuomba Mahakama yenye mamlaka ya kusikikiza kesi ya uhaini na Mahakama yenyewe ndiyo hii tuliyopo.”

Lissu katika pingamizi anadai mashahidi aliowataja lakini hawakuorodheshwa ni Samia Suluhu Hassan, Dk Philip Mpango na Kassim Majaliwa. Samia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nayemaliza muda wake, Dk Mpango ni Makamu wa Rais na Majaliwa ni Waziri Mkuu.

Wakili Mrema alidai Rais na viongozi aliowataja wana kinga ya kuwa mashahidi kwa mujibu wa sheria ya masuala ya urais kifungu cha 10 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Kupitia kifungu hicho, amedai utaratibu umeainishwa wazi na ndiyo maana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haikuwaorodhesha.

Kutokana na majibu hayo, aliomba mahakama itupilie mbali pingamizi la Lissu na ikubaliane na hoja za upande wa mashtaka.

‎Akijibu hoja za Jamhuri kuhusu sheria ya masuala ya uraisi ya mwaka 1962, alisema sheria hiyo inasema kuna taratibu ambazo zinatakiwa kufanywa ili rais aweze kuitwa kutoa shahidi katika kesi.

Alidai taratibu hizo ni pamoja na kupeleka wito wa mahakama kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu Mkuu au Katibu wa Rais na hao wote watatoa msaada.

Alidai kuwa Raisi ana kinga ya kutokushtakiwa tu na si ya kuitwa kutoa ushahidi.

Amedai sheria ‎mashauri yanayofunguliwa mahakama za chini kwa hatua za awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ni tofauti na mengine kwa ujumla wake.

Kwa mujibu wa Lissu, mwenendo wa kuhamisha kesi unataka mtuhumiwa ashtakiwe katika eneo alikokamatiwa na si wapi kosa lilitendeka, kwa mujibu wa kifungu cha 262(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai.

Amedai katika mazingira hayo, mahakama iliyokuwa na mamlaka ya kuendesha mwenendo huo ni Mbinga alikokamatwa na si Kisutu alikoshtakiwa.

‎Akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, Lissu amedai mahakama hiyo ilisema ili Mahakama Kuu ipokee na kusikiliza shauri la aina hiyo, sharti liwe limekabidhiwa kwake kwa mujibu wa sheria.

‎Kuhusu mwenendo wa kuhamisha kesi kukiuka vifungu vya sheria, Lissu amedai kifungu cha 266 (3) liko wazi kuhusu nyaraka ambazo mshtakiwa anapaswa kupewa kuwa ni hati ya mashtaka, hati za maelezo na kumbukukmu zote za shauri husika.

‎‎Hata hivyo, amedai alipewa wa siku moja Agosti 18, 2025, wakati kumbukumbu za mahakama na walizonazo upande wa mashtaka zina kurasa 101.

‎‎Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka hilo Aprili 10, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya taratibu za awali, kabla ya kesi kuhamishiwa Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kuisikiliza.

Anadaiwa akiwa raia wa Tanzania, alishawishi umma kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania.

‎‎‎Agosti 18, 2025 Mahakama ya Kisutu baada ya kukamilisha jukumu lake iliihamishia kesi hiyo Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji.