Nzega. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznia kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuyafanyia kazi maombi yaliyowasilishwa kwake na mgombea ubunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, ikiwemo kuanzisha mkoa mpya wa Nzega.
Samia ametoa ahadi hiyo leo, Septemba 10, 2025, wakati wa mkutano wake wa kampeni katika Jimbo la Nzega Mjini mkoani Tabora, baada ya kupokea maombi hayo kutoka kwa Bashe.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Bashe amemuomba mgombea huyo, katika awamu yake ijayo endapo atachaguliwa, augawe Mkoa wa Tabora ili wapate mkoa mpya wa Nzega.
Amesema Mkoa wa Tabora ni mkubwa ukiwa na idadi ya watu zaidi ya milioni tatu, hivyo ni muhimu kuugawa ili kuwarahisishia wananchi huduma za kiutawala na kijamii katika maeneo ya karibu yao.
Amesema mkoa wa Nzega ukichukua maeneo ya Uyui, Nzega Vijijini, Bukene na Igunga, ukanda huo utakuwa na watu milioni 1.8, na amesisitiza kwamba inatosha kuanzisha mkoa mpya.
“Tunaomba tuwe na Mkoa wa Nzega, ni jambo ambalo tumelilia kwa muda mrefu na itakuwa ni heshima kubwa kwako. Nikutoe wasiwasi, hakutakuwa na gharama za utawala, bali utarahisisha huduma kwa wananchi hawa,” amesema mgombea huyo.
Bashe ameomba pia Bukene na Manonga, kila moja iwe na halmashauri yake ili kuchochea maendeleo kwa wananchi wa eneo hilo, huku akimtoa hofu kwamba hilo haitakuwa na gharama kubwa za kiutawala.
Vilevile, mgombea huyo wa ubunge ameomba kuanzishwa kwa tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mji wa Nzega ili kuwasaidia wananchi wanaotoka katika ukanda huo kupata elimu bora katika mazingira yao.
Akijibu maombi hayo ya Bashe, Samia amesema ameyachukua yote na atakwenda kuyafanyia kazi ili kubaini kama kuna uhitaji huo.
“Amewasilisha hapa maombi matatu na yote tunakwenda kuyafanyia kazi… la halmashauri, nakwenda kulifanyia kazi, la kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwepo Nzega, nakwenda kulifanyia kazi na hili la mkoa, nakwenda kuliangalia kwa undani zaidi. Kwa hiyo, tunakwenda kuyafanyia kazi, jawabu ni mbili, ndiyo au siyo, inawezekana au haiwezekani, lakini tumeyapokea, tunakwenda kuyafanyia kazi,” amesema Samia kwenye mkutano huo.
Amempongeza Bashe kwa kazi nzuri anayoifanya kama Waziri wa Kilimo na kwamba ameibeba sekta ya kilimo kwa moyo wake wote, na kwamba inasemekana hakuna waziri mchapakazi aliyewahi kutoka katika wizara hiyo.
Akizungumzia maendeleo katika jimbo lake, Bashe amesema miaka mitano iliyopita, maji katika mji wa Nzega yalikuwa yanauzwa Sh500 kwa dumu moja, na upatikanaji wake ulikuwa mdogo kwani walifuata umbali mrefu.
“Kata zote 10 na vijiji vyote 21 vina maji. Dumu la maji tulilokuwa tunanunua Sh500, unit moja ya maji tunanunua Sh1,500, unit moja ni sawa na lita 1,000 ambazo mwananchi angenunua kwa Sh25,000,” amesema.
Amesema wananchi wa vijijini ndiyo wanaelewa mambo hayo. Amesema kaya zote 14,000 katika mji wa Nzega zimeunganishwa na huduma ya maji, walianza kulipia asilimia 10 ya fedha walizotakiwa kulipia, ambazo ni Sh300,000 ili kuunganishiwa maji, na sasa kila mmoja amemaliza deni lake.
“Tunaenda kukuchagua kwa sababu umefanya mambo ambayo katika nchi hii hayakuwahi kufanyika tangu uhuru. Kwetu wewe ni mkombozi wetu, umetufanyia mengi makubwa,” amesema.
Wengine waeleza mafanikio
Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukene, John Luhende, ameomba kujengwa kwa barabara ya lami kutoka Nzega kuelekea Bukene ili kuunganisha maeneo hayo na kuwawezesha wananchi kusafirisha mazao yao.
Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwasaidia wananchi kupitia skimu za umwagiliaji, kwani wengi wao wanategemea kilimo, hivyo ameomba kuongezwa kwa skimu nyingi zaidi ili wakulima wazalishe wakati wote.
“Tunashukuru kwa mengi ambayo Serikali imeyafanya katika jimbo, tuna uhakika wananchi wanakwenda kutuchagua tena kwenye uchaguzi ujao,” amesema mgombea huyo.
Mgombea ubunge wa Nzega Vijijini, Neto Kapalata, amesema katika jimbo hilo kuna miradi mingi ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa.
“Oktoba 29, 2025 tunakwenda wote kukupigia kura uendelee kuwa Rais wetu. Kazi umeifanya, wananchi wameona, tukuombe tu utusaidie skimu za umwagiliaji zije kwa haraka,” amesema.