Kaliua. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimesema endapo kitaingia madarakani, kitahakikisha wakulima wa tumbaku wanapata manufaa halisi ya kilimo hicho kwa kuondoa changamoto zinazowakwamisha, ikiwamo udhibiti wa madalali wanaowanyonya.
Chama hicho pia kimeahidi kuweka mifumo bora ya ununuzi wa tumbaku na kuhakikisha bei ya mazao inaakisi gharama halisi za uzalishaji ili kuongeza tija kwa wakulima na kuinua uchumi wa maeneo yanayolima zao hilo.
Kimesema hakuna mikakati ambayo Serikali iliyopo madarakani imeweka ili wakulima wa zao hilo wanufaike, badala yake wawekezaji wamekuwa wakilichezea zao hilo.
Mikakati hiyo ya Chaumma imelenga kuinua zao hilo ambalo Ripoti ya Takwimu za Msingi Tanzania 2023 inaonesha kuongezeka uzalishaji nchini.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonesha, kukua kwa mauzo kutoka Sh291.4 bilioni mwaka 2021 hadi Sh824.9 bilioni mwaka 2023 ya zao hilo kunaifanya tumbaku kushika nafasi ya pili katika mauzo ya bidhaa za asili nje ya nchi na kuleta mapato mengi nchini
Kauli hiyo ya Chaumma, imetolewa leo Septemba 10, 2025 katika Kata ya Kaliua mjini mkoani Tabora na mgombea mwenza urais, Devotha Minja wakati akinadi sera za chama chake kipate kuaminiwa na wananchi kiunde Serikali.
Mgombea mwenza huyo amesema, ifike mahai wakulima wa Tanzania wapewe heshima inayostahili,”leo naambiwa ili uuziwe tumbaku lazima utoe rushwa, yaani madalali waseme hii peleka hii usipeleke, mkulima anahangaika kulima peke yake, mbolea ni ya mateso.
“Kulima shamba ni gharama kubwa, viuatilifu gharama halafu mtu anakuja kukuambia toa rushwa ili uuze, haiwezekani huu ni mfumo ambao kama haubarikiwi nkwa nini hawa madalali hawachukuliwi hatua,” amesema.

Mgombea mwenza huyo, ameowaomba wananchi kukiamini chama hicho, ili kundi la madalali wa zao la tumbaku wakaondolewe.
Minja amesema, zao la tumbaku haliwezi kubadilisha maisha ya wananchi kama halikusimamiwa vizuri, akieleza kuwa wawekezaji wamekuwa wakilichezea chezea tu.
Amesema Kaliua wanalima zao hilo na viwanda vyake vipo Mkoa wa Morogoro,
“Hatusemi ni vibaya, lakini viwanda viendane na mahala husika, kama mnalima tumbaku na kiwanda chake kiwe hapa ili vijana wenu wapate ajira,” amesema.
Amesisitiza, wakulima wanapaswa kufahamu mambo yanayohusiana na tumbaku eneo walipo na haiwezekani kupanda mabasi kwenda kuuliza mambo hayo mkoani Morogoro kulipo na viwanda.
Minja amesema kinachofanywa na Serikali kimedhamiria kuwaumiza wakulima wa zao hilo, kwa namna ambavyo hakuna mbinu ya kuwainua wakulima.
Mgombea udiwani Kata ya Kaliua Mjini, Lutas Mathew amesema vyama vya ushirika vipo kwa ajili ya kuwaumiza wakulima na akipata ridhaa atahakikisha wananchi wanaondokana na mifumo kandamizi kwenye kilimo.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kaliua, Ramadhani Lusaku amesema atahakikisha Jimbo la Kaliua linaunganishwa kwa lami hadi Mpanda.
“Nitakachofanya nitawaletea maendeleo kinamama wanaosumbuliwa na michango, nitapambana kwa ajili ya wananchi wa Kaliua nitashirikiana nanyi bega kwa bega, huu ushuru wa kila gunia la mazao yetu kutozwa Sh1,000 tutakomesha,” amesema.