Simba yalipa kisasi kwa Gor Mahia

TAMASHA la Simba Day limehitimishwa kwa mechi ya kirafiki wa kimataifa uliozikutanisha Simba dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

Mchezo huo uliofanyika leo Septemba 10, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba imeibuka na ushindi wa mabao 2-0, huku ikilipa kisasi mbele ya Gor Mahia.

Kisasi hicho Simba imelipa baada ya mara ya mwisho kukutana kwao Juni 10, 2018 katika fainali ya SportPesa Super Cup ambapo Gor Mahia ilishinda pia 2-0 kwa mabao ya Meddie Kagere dakika ya 6 na Jacques Tuyisenge dakika ya 55.

Katika mchezo wa leo, Simba ilipata bao la kwanza dakika ya 6, baada ya Abdulrazack Hamza kuunganisha kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na Jean Charles Ahoua.

Bao hilo la mapema lilifanya mashabiki wa Simba waliojitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa kushangilia kwa nguvu na kuendelea kuwapa sapoti mastaa wao.

Mbali na kushangilia bao hilo, pia ufundi wa baadhi ya mastaa wa Simba waliouonesha ndani ya uwanja wakiwemo wapya kama Naby Camara na Rushine De Reuck, ulikuwa kivutio tosha. Mwingine ni kipa Yakoub Suleiman aliyeingia dakika ya 31 kuchukua nafasi ya Moussa Camara.

Wakati Simba ikiwa mbele kwa bao moja, Gor Mahia ilirudi mchezo na kupangilia mashambulizi, lakini eneo la ushambuliaji lililokuwa likiongozwa na Christopher Ochieng halikuwa makini.

Kipindi cha kwanza, Simba ilikwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa bao 1-0. Iliporejea kipindi cha pili, Kocha Fadlu Davids alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu, akiwatoa Chamou Karaboue, Jonathan Sowah na Kibu Denis, nafasi zao zikachukuliwa na Yusuph Kagoma, Elie Mpanzu na Steven Mukwala.

Mukwala alitumia dakika tatu pekee akiwa uwanjani kufunga bao la pili lililoongeza furaha Msimbazi. Hata hivyo, mshambuliaji huyo ilipofika dakika ya 65, zikiwa ni dakika 20 tangu aingie, alitolewa na kuingia Seleman Mwalimu.

Mbali na mabadiliko hayo, Fadlu pia aliwapa nafasi nyota wengine walioingia kipindi cha pili ambao ni Joshua Mutale, Morice Abraham, David Kameta ‘Duchu’, Vedastus Masinde, Wilson Nangu, Alassane Kante, Mzamiru Yassin, Alexander Erasto na Bashir Salum.

Kwa ushindi huo, Simba imeendelea kuwa na wakati mzuri katika Tamasha la Simba Day tangu 2009 ambapo sasa imeshinda michezo 12 ya kirafiki.

Katika historia ya michezo ya Simba Day kuanzia mwaka 2009 hadi sasa 2025, Simba imeshinda dhidi ya SC Villa (2009, 2013 na 2015), AFC Leopards (2016), Rayon Sports (2017), Asante Kotoko (2018), Power Dynamos (2019 na 2023), Vital’O (2020), St George (2022), APR (2024) na Gor Mahia (2025).

Pia imetoa sare moja pekee dhidi ya Express mwaka 2010, huku ikipoteza michezo minne dhidi ya Victors (2011), Nairobi City Stars (2012), Zesco United (2014) na TP Mazembe (2021).