Sowah awa gumzo  mapema Simba Day

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, raia wa Ghana, Jonathan Sowah amegeuka gumzo mapema kwa mashabiki wa timu hiyo walihudhuria katika tamasha la Simba Day, linalofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika mitaa mbalimbali ya nje ya uwanja huo, mashabiki wa timu hiyo wanazungumzia usajili wa nyota wapya msimu huu, huku Sowah akibeba matumaini zaidi kutokana na ubora alionao wa kufunga mabao.

Shabiki wa Simba aliyejitambulisha kwa jina la Dickson John, amesema licha ya usajili bora uliofanyika msimu huu, ila kwake amevutiwa na Sowah.

“Jamaa ana nguvu na anajua kupambana, hata akiwa na zaidi ya mabeki wawili ana uwezo wa kuwapita, ni mchezaji ninayejivunia nikiamini atatusaidia sana katika eneo la ushambuliaji,” amesema Dickson.

Kwa upande wa shabiki mwingine aliyejitambulisha kama ‘Van JR’, amesema usajili wa msimu huu wa Simba unaashiria ni mwaka wa kurejesha heshima ya kikosi hicho ya kuchukua mataji mbalimbali hususani Ligi Kuu Bara iliyoyakosa kwa misimu minne.

Kwa upande wa Asnath Jeshi, amesema kikosi cha msimu huu kimekamilika kila eneo hivyo hana shaka na wachezaji wote akiamini wataipambania nembo ya klabu hiyo katika mashindano mbalimbali msimu wa 2025-2026.

Sowah amejiunga na timu hiyo akitokea Singida Black Stars, huku nyota huyo akifunga mabao 13 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025.