Ukata watajwa kukwamisha kampeni za vyama vya upinzani Mbeya

Mbeya. Zikiwa zimetimia siku 14 tangu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuruhusu kuanza kwa kampeni, baadhi ya vyama vya siasa, hususani vya upinzani mkoani Mbeya bado hakijaeleweka, huku wagombea wakieleza sababu tofauti.

INEC ilitangaza kuanza kampeni za uchaguzi mkuu tangu Agosti 28 kwa wagombea nafasi za urais, ubunge, udiwani na uwakilishi, lakini kwa Mkoa wa Mbeya ni CCM pekee waliofanya hivyo kwa mgombea urais, Samia Suluhu Hassan.

Pia, upande wa ubunge tayari baadhi ya majimbo wameshazindua kampeni zao, ikiwa ni Rungwe, Busokelo na Chunya, huku Uyole ikitarajiwa Septemba 13, Mbeya Mjini Septemba 14 na Mbarali na Mbeya Vijijini Septemba 15.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Septemba 10, 2025 baadhi ya vyama vya siasa wakiwamo wagombea nafasi za ubunge wamesema ukata na ratiba ndizo zinazowakwamisha, huku wakiahidi kabla ya muda kuisha kufanya hivyo.

Mgombea ubunge Jimbo la Uyole kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Mwakwama amesema ukata ndio sababu kubwa iliyochelewesha kuanza kampeni, akiahidi kuwa hivi karibuni atafanya hivyo.

“Nilitarajia kuzindua Septemba 14, lakini tarehe hiyo kutakuwa na mgombea urais wa chama cha DP, hivyo hairuhusiwi. Hivyo natarajia Septemba 19, lakini kubwa zaidi ni masuala ya fedha yanatatiza,” amesema Mwakwama.

Amefafanua kuwa kampeni za chini kwa chini zinaendelea, isipokuwa anaendelea kujipanga kwa ajili ya mkutano wa hadhara, akieleza kuwa mkutano mmoja unagharimu takribani Sh500,000.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa chama cha ACT-Wazalendo, Malongo Wailes amesema alitarajia kuzindua leo Septemba 10, lakini amepokea waraka kutoka makao makuu kusubiri hatima ya mgombea urais wa chama hicho, Luhaga Mpina.

“Nilijipanga leo, lakini kuna maelekezo kutoka juu kusubiri hatima ya mgombea wetu wa urais kuhusu hatima yake kesho mahakamani ili kujua uamuzi wa Mahakama,” amesema Wailes.

Katibu wa chama cha ADC, Godfrey David amesema pamoja na wagombea wake kutozindua kampeni, bado wapo ndani ya siku 60 zilizoelekezwa na INEC kuhusu kampeni.

“Nina wagombea wawili nafasi za udiwani Mbarali na Kyela, kutofanya kampeni hadi sasa ni suala la maandalizi na bado muda upo, tunafanya mipango kwa ajili ya shughuli hiyo,” amesema David.

Mchambuzi wa siasa jijini Mbeya, Elisha Michael amesema kuchelewa kwa kampeni za wagombea kunaweza kuwa ni kutokana na uchumi wa vyama na kupotea kwa ushindani kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

“Kuna baadhi ya majimbo wagombea ni chama kimoja, lakini unakuta sehemu walipo wapinzani nguvu yao kifedha ni ndogo, hali inayofanya mvuto na ushindani wa kisiasa kupotea,” amesema mdau huyo wa siasa.