Na Mwandishi Wetu,Mkuranga
MGOMBEA ubunge Jimbo la Mkurunga mkoani Pwani Abdallah Ulega, ameendelea kuimarisha kampeni zake kwa kunadi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030 huku akisisitiza dhamira ya chama hicho ni kuendelea kuboresha maisha ya wananchi na ustawi wa maendeleo.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Kata ya Vikindu, Ulega, ambaye aliainisha mikakati ya CCM na serikali ijayo chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepanga kutatua changamoto za wananchi.
Amesema miongoni mwa maeneo ambayo yameelezwa kwa kina katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ni miradi ya maji, elimu, afya, barabara pamoja na uboreshaji wa fursa za kiuchumi kwa vijana na wanawake.
Pia Ulega amewanadi na kuwaombea kura wagombea udiwani wa kata mbalimbali za wilaya hiyo ambapo amebainisha mshikamano kati ya mbunge, madiwani na serikali kuu ndio nguzo ya maendeleo ya kweli kwa wananchi.
Awali Meneja wa Kampeni za CCM Jimbo la Mkuranga, Juma Abeid, aliwaeleza wananchi wa Vikindu namna serikali ya Rais Samia imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akiweka mfano wa Kata ya Magawa, Abeid ameeleza miradi mingi ya kijamii imepokea ufadhili kutoka serikalini, jambo linaloonyesha dhamira thabiti ya Rais Samia kuwaletea wananchi maendeleo yenye tija.
Hivyo ametumia mkutano huo kumuombea kura nyingi Dkt. Samia, kura nyingi kwa Ulega, pamoja na Diwani ili kuendeleza kazi iliyobaki ya kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo,” alisema Abeid huku akishangiliwa na wananchi.
Wananchi waliokuwepo kwenye mkutano huo walionesha hamasa kubwa na kuahidi kuiamini CCM kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyokwisha kufanyika, hususan katika sekta za elimu, afya na miundombinu ya barabara vijijini.