Vifo vya kujiua vyageuka tishio

Dodoma/Dar.  Wakati Tanzania ikiadhimisha siku ya kuzuia kujiua duniani, imeelezwa idadi ya wanaojiua nchini inaongezeka, wanaume wakiongoza.

Kuokana na hilo, mamlaka zinazohusika zimetakiwa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, jitihada kadhaa zinachukuliwa zikiwamo kampeni za uhamasishaji, kuboresha huduma za ushauri katika vituo vya afya na kuanzisha namba maalumu ya msaada wa kisaikolojia bure (199), hivyo wananchi wanaweza kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi (sms).

Utafiti uliofanywa na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, unaonesha vifo 1,141 vilivyotokana na kujiua vilitokea mkoani humo kuanzia Januari  2024 hadi Juni 2025, huku wanaume wakiongoza kwa asilimia kubwa.

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Septemba 10, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mirembe, Dk Paul Lawala jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani.

Amesema idadi hiyo ni kubwa na inazidi kuongezeka siku hadi siku, hivyo mamlaka zinazohusika zichukue hatua za haraka.

Dk Lawala amesema Hospitali ya Mirembe baada ya kuona idadi ya matukio ya watu kutaka kujiua, kutishia kujiua na kujiua yameongezeka waliamua kufanya utafiti kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na kupata idadi hiyo ya watu kujiua katika kipindi cha miezi 18.

“Asilimia kubwa ya watu wanaojiua ni wanaume kwa sababu wana mambo mengi wanayokabiliana nayo lakini hawataki kuyaongea, tofauti na wanawake ambao ni wepesi kuzungumza. Wanapozungumza hupata msaada unaowaepusha na kujiua, ndiyo maana idadi yao ni ndogo kulinganisha na wanaume,” amesema Dk Lawala pasipo kutaja takwimu hizo.

Mbali ya hayo, taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa leo Septemba 10 na kusainiwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, imeeleza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kupambana na kujiua.

Jitihada hizo ni  kampeni za uhamasishaji, kuboresha huduma za ushauri katika vituo vya afya na kuanzisha namba maalumu ya msaada wa kisaikolojia bure (199) ambayo wananchi wanaweza kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi (sms) kwenda 15061 ili kupata ushauri.

Dk Lawala amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha  mwaka 2018 watu 3,000 walijiua nchini Tanzania kwa sababu mbalimbali, huku takwimu za kidunia zikionesha watu 720,000 duniani hujiua kila mwaka.

Amesema changamoto ya watu kujiua inashika nafasi ya tatu nchini kwa kusababisha vifo, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha anajiweka mbali na visababishi vya kujitoa uhai ikiwamo ulevi kupindukia, sonona, matumizi ya dawa za kulevya, ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na magonjwa sugu.

Dk Lawala ametaka sheria za makosa ya jinai zipitiwe upya, akieleza mtu akibainika alitaka kujiua anaadhibiwa kisheria, kwani kosa hilo siyo la jinai bali ni matatizo ya afya ya akili ambayo yanahitaji tiba na siyo kumfunga mtu.

Akizungumzia sababu za wanaume wengi kujiua, Said Kuganda, daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) amesema matarajio ya kijamii yana mchango.

“Kitamaduni, wanaume wanatarajiwa kuwa wenye nguvu na wasioneshe hisia. Hali hii huwazuia kufunguka kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo, hivyo kuwasababisha kuwa katika hatari zaidi. Wanawake wanaweza kujaribu kujiua mara nyingi zaidi, lakini majaribio ya wanaume mara nyingi huwa na matokeo ya vifo,” amesema.

Daktari bingwa wa afya na magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Mirembe, Veronica Lyimo, amesema makundi yaliyopo hatarini kujiua ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 29 na kundi la watu wazima wenye umri kuanzia miaka 45 na kuendelea.

Amesema nchi zinazoathirika zaidi na tatizo la kujiua kwa asilimia 75 ni zenye uchumi wa kati na uchumi wa chini, tofauti na zenye uchumi wa juu, ambazo matukio ya kujiua si mengi.

Amesema mara nyingi watu hujitoa uhai kwa ama kutumia sumu, silaha au kujinyonga.

“Pamoja na kwamba nchini kuna watu wanaomiliki silaha, lakini njia inayotumiwa na wengi ni sumu na kujinyonga. Takwimu pia zinaonesha wanaume wengi wakifanya uamuzi wa kujiua hufanikiwa kuliko wanawake,” amesema.

Dk Lyimo amesema wanawake ni wepesi kueleza matatizo yao na kupata msaada tofauti na wanaume, ambao kiasili wamejengewa ujasiri wa kuyabeba mambo na kupambana kiume kwa hiyo ni sababu ya wengi wao kujitoa uhai.

Amesema sababu nyingine ya watu kujiua ni kutokana na maumivu makali mwilini yanayosababishwa na magonjwa sugu au ya kudumu, ambayo husababisha wajiue ili kuondokana na mateso ya magonjwa hayo yakiwamo ya akili, sonona, kiwewe na matumizi ya dawa za kulevya.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, amesema wakati kila sekunde 40 kuna mtu anajiua duniani, watumishi wa sekta mbalimbali, wamo hatarini zaidi.

“Nilifanya utafiti nikagundua wengi hujiua kwa kujinyonga, kunywa sumu za shambani, dawa kwa ku-over dose (kuzidisha kiwango kinachotakiwa). Nusu ya Watanzania wanamiliki simu na wana makundi sogozi. Hawana muda wa kukutana kuzungumza,” amesema.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye idadi kubwa ya matukio ya watu kujiua, zingine ni Afrika Kusini, Botswana, Nigeria na Uganda.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Thomas Rutachunzibwa amewataka wataalamu na wahudumu wa afya kuisaidia jamii isifikie hatua ya kujitoa uhai kwa kutoa huduma bora za matibabu na kutoa faraja kwa wagonjwa.

Amesema migogoro ya ndoa na uhusiano, mazingira mabaya ya kazi na kuyumba kiuchumi yanaweza kusababisha mtu kujitoa uhai kama hatua za haraka hazitachukuliwa.

Amewataka watumishi wa afya mkoani Dodoma kuwa na vyanzo mbadala vya mapato badala ya kutegemea ajira peke yake ili kujiepusha na sonona inayoweza kusababisha wafikirie kujitoa uhai.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Delila Kimambo amesema pamoja na hospitali hiyo kutoa huduma kwa wenye changamoto ya afya ya akili, wafanyakazi wa afya ni muhimu kuangaliwa.

Kufuatia hilo, amezindua kliniki mahususi ya afya ya akili kwa ajili ya wafanyakazi wa hospitali hiyo inayolenga kutoa huduma za ushauri, uchunguzi na tiba ya changamoto za kisaikolojia, ikiwamo mfadhaiko na msongo wa mawazo unaoweza kuchochea tabia za kujiua.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa na kimataifa wa kudhibiti ongezeko la matukio ya kujiua na majaribio yake.

“Tumeona ni muhimu kuwapa kipaumbele wafanyakazi wetu kwani wao ndio nguzo ya huduma za afya. Kliniki hii itasaidia kuondoa unyanyapaa, kutoa msaada wa haraka na kuimarisha afya ya akili ili kuhakikisha kila mmoja anahisi kuthaminiwa na kuungwa mkono,” amesema.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Magembe amesema Wizara ya Afya inatoa wito kwa jamii nzima kuwa sehemu ya suluhisho katika kupambana na tatizo la kujiua.

“Tujifunze kusikiliza bila kuhukumu, kuonyesha upendo na huruma kwa wale wanaopitia changamoto za afya ya akili na kuwahimiza kutafuta msaada mapema. Tujenge mazingira salama ya kuzungumza wazi bila aibu, na tuondoe dhana ya unyanyapaa dhidi ya matatizo ya akili ndani ya jamii zetu. Kila mmoja ana jukumu la kulinda na kuthamini maisha, tuungane kuleta tumaini kupitia vitendo,” amesema.