WAKATI biashara mbalimbali zikiendelea kufanywa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa linapofanyika tamasha la Simba Day leo, wapiga picha mnato nao wameanzisha ubunifu wa kuhakikisha wanajipatia pesa katika siku hii kubwa kwa mashabiki wa Simba.
Badala ya kupiga picha tu za mashabiki wakiwa wamekaa sehemu tofauti tofauti, sasa wameamua kuweka mabango ambayo shabiki anayehitaji atapigwa picha hapo.
Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja ya wapiga picha hao amesema gharama ya kupiga picha kwenye bango hilo lenye picha za wachezaji wa Simba ni shilingi elfu mbili.
“Gharama hii ni tofauti ikiwa shabiki atahitaji kupiga picha bila ya bango hilo, ikiwa atapiga picha bila ya bango atalipa 1500,” amesema mpiga picha aliyejitambulisha kwa jina la Mashaka Ramadhani.
Idadi kubwa ya mashabiki tayari imeshawasili uwanjani hapa, wengi wao wakiwa tayari wameshaingia uwanjani.
Tamasha hilo la 17 linafanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, linalotumika kutambulisha nyota wapya sambamba na kikosi kipya cha Wekundu hao kwa msimu mpya wa mashindano wa 2025-2026 na saa 1:30 usiku itahitimishwa na pambano kati ya timu hiyo na Gor Mahia ya Kenya.