Wakazi Bonde la Mto Msimbazi waliamsha tena kutaka fidia

Dar es Salaam. Wakazi wa Jangwani waliopisha mradi wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, jijini Dar es Salaam wameibua upya madai yao, wakikumbusha haki ya kulipwa fidia ya ardhi kwa mujibu wa sheria, baada ya maeneo yao kutwaliwa kwa ajili ya mradi huo.

Mradi huo, unaotekelezwa chini ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), unalenga kukabiliana na mafuriko na kuboresha matumizi ya ardhi katika maeneo ya chini ya bonde hilo.

Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya takribani Sh598 bilioni, na umeathiri zaidi ya wakazi 2,600. Kwa awamu ya awali, Sh52.6 bilioni zilitengwa kwa ajili ya fidia kwa wakazi waliopisha mradi huo.

Hata hivyo, madai yameibuka upya licha ya Serikali kutoa malipo ya Sh4 milioni kwa kila mkazi kwa ajili ya kutafuta ardhi mbadala, tangazo lililotolewa na Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa, Novemba 15, 2023.

Katika mkutano uliofanyika viwanja vya Jangwani, Waziri Mchengerwa alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alisikiliza kilio cha wananchi na kuagiza walipwe kiasi hicho, kwa kuwa eneo walilokuwa wanaishi ni oevu na hivyo kisheria halistahili fidia ya ardhi.

Malipo hayo, yaliyotolewa kuanzia Novemba 16, 2023, yalihusisha kifuta jasho, fidia ya usumbufu, mali, pamoja na kodi ya nyumba ya miaka mitatu kwa waliokuwa wakiishi katika eneo hilo.

Pamoja na hayo, baadhi ya wakazi wameendelea kuwasilisha barua za malalamiko wakitaka walipwe fidia ya ardhi, wakidai hawajatendewa haki.

Hata hivyo, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), ambao ni wasimamizi wa utekelezaji wa mradi huo, wamesisitiza kuwa malipo yaliyotolewa ni ya haki na kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Mratibu wa Mradi, Humphrey Kanyenye, amethibitisha kupokea barua nyingi kutoka kwa wananchi, baadhi zikielekezwa hadi Benki ya Dunia.

Hata hivyo, amesema baada ya kupitia malalamiko hayo, hakuna hoja mpya zenye msingi, kwani wananchi walishirikishwa katika kila hatua na nyaraka zote zipo kwa uthibitisho.

“Katika miradi kama hii malalamiko hayakosekani, lakini kwa bahati mbaya sana hao wanaolalamika katika mradi huu, zikipitiwa barua zao wanaonekana hawana hoja na uzuri kila kitu tulichofanya nao kipo katika maandishi,” amesema Kanyenye.

Ni kutokana na hilo, amesema, ndio maana hata utekelezaji wa mradi wenyewe umeshaanza na sasa kunajengwa madaraja, huku kuanza kujengwa kwa mto kukitarajiwa kuanza Novemba mwaka huu baada ya mkandarasi kupatikana.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mwenyekiti wa wakazi wa Jangwani, Saleh Cheyo, amesema kuwa wakati wa upimaji wa maeneo yao kwa ajili ya kupisha mradi wa Bonde la Mto Msimbazi, waliandikishwa kwa mujibu wa vipimo vya ardhi na majengo yao.

Hata hivyo, Cheyo ameonesha kushangazwa na hatua ya wasimamizi wa mradi huo kurudisha fomu za malipo zilizoonesha fidia ya jengo pekee, huku wakipuuzia thamani ya ardhi.

Aidha, amedai kuwa kiwango cha fidia kilichowekwa hakilingani na thamani halisi ya nyumba zao, na kwamba walilazimishiwa kukubali kiasi kilichoamuliwa na wasimamizi badala ya thamani halisi iliyopimwa.

“Baada ya kufuatilia tunavyopaswa kulipwa ni pamoja na ardhi, lakini kwa bahati mbaya hata ukiwakumbusha mara kwa mara kuhusu kutulipa hela yetu hii, wamekuwa wakituzungusha na ndio maana tumeamua tupaze sauti yetu kupitia vyombo vya habari, huenda mamlaka zikatusikia,” amesema Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo, Cheyo amesema Sh4 milioni zilizotolewa kama kifuta jasho cha ardhi, wengi walichukua tu kwa shingo upande, huku baadhi kwa uelewa wao mdogo wakaona ni hela nyingi na kuzichukua.

Pamoja na hilo, amesema ukweli ni kwamba kiasi hicho cha fedha kwa jiji la Dar es Salaam huwezi kupata ardhi mbadala na kujenga nyumba, zaidi utaishia kwenda kujenga tena mabondeni.

Naye mkazi mwingine, Abdul Banzi, amesema awali katika vikao vyao na wasimamizi wa mradi walikubaliana kulipwa kila kitu kitakachokutwa katika eneo lao, na baada ya fomu kurudishwa na kuhoji hilo, walijibiwa kuwa zinafanyiwa kazi na kuwataka wavute subira.

“Baada ya kuambiwa hivyo nasi tukasubiri, lakini subira ina mwisho wake katika mtu kupata haki yako, ndio maana leo tumeamua kukusanyika hapa kujadiliana na kuzikumbusha mamlaka madai yetu hayo,” amesema Banzi.

Denis Mhanda, mmoja wa waliopisha mradi huo, amesema mwaka 2021 maofisa wa Serikali walifika katika eneo lao na kutoa ahadi nzuri kuhusu mradi huo na namna wangelipwa fidia stahiki.

Hata hivyo, anasema waliporejea mwaka 2023 na nyaraka za malipo, hali ilikuwa tofauti na makubaliano ya awali.

“Kila tukiwahoji kuhusu tofauti hiyo huambiwa tusubiri au kupewa tarehe nyingine bila majibu ya msingi,” amesema Mhanda.

Ester Abdallah, naye mkazi wa eneo hilo, amesema awali walifurahi kusikia juu ya ujio wa mradi kwa kuwa walidhani utawaletea neema, lakini hali imekuwa tofauti.

“Tulielezwa kuwa hatustahili kulipwa fidia ya ardhi kwa sababu ni eneo oevu, lakini huo si ukweli. Barabara ya lami imepita hapa na watu walilipwa, pia kuna kituo cha mabasi ya mwendo kasi na hata bandari bubu, yote hayo yamejengwa kwenye eneo hilo. Kama ni oevu, kwa nini hayo yakaruhusiwa?” amehoji Ester.

Ameongeza kuwa fedha waliyopewa ni ndogo kiasi kwamba haiwezi kuwasaidia kujenga upya wala kuanza maisha sehemu nyingine kwa heshima.