Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema ni marufuku kwa mkulima yeyote wa zao la kahawa kung’oa miti ya kahawa bila kuwa na kibali rasmi kutoka kwa mkuu wa wilaya husika, akisema hatua hiyo inalenga kulinda zao hilo.
Babu ametoa agizo hilo leo, Septemba 10, 2025, wakati wa uzinduzi wa tamasha la kahawa maarufu ‘Kahawa Festival 2025’ msimu wa Sita. Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi uliopo makao makuu ya Bodi ya Kahawa (TCB) mjini Moshi.
Amesema kuwa Serikali ya mkoa huo haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayekiuka agizo hilo, kwa kuwa zao la kahawa ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato kwa wakulima na mkoa kwa ujumla.
“Fahari yetu sisi wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro ni zao la kahawa, lakini leo kwenye familia zetu kuna watu wanakata miti ya kahawa ili ajenga nyumba, hili jambo halitatufikisha mahali pazuri.
“Ni marufuku kukata zao la kahawa. Ukikata kahawa ya zamani aliyootesha babu yako upande wa miche mingine bila kufanya hivi, hatuwezi kwenda. Hata kama mti huo umeupanda wewe, ni marufuku kukata mpaka upewe kibali na Mkuu wa Wilaya,” amesema na kuongeza;
“Jamani, zao letu kuu la Mkoa wa Kilimanjaro ni kahawa. Ukiacha ndizi na mazao mengine, tukiamua mimi na nyie tunaweza. Nimeambiwa kahawa sasa hivi kilo moja ni Sh12,000, nikauliza heka moja ya shamba unapanda kahawa kiasi gani nikaambiwa miche 540; ukiutunza vizuri unapata faida ya kutosha.”
Amesema tayari Serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta hiyo ya kahawa kwa kuongeza huduma za ugani, pembejeo na miundombinu ya umwagiliaji, na hivyo uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutoka asilimia 37 hadi 42 kwa mwaka.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa nchini (TCB), Primus Kimaryo, amesema tamasha hilo limelenga kuhamasisha unywaji wa ndani wa kahawa ili kukuza soko la ndani la zao hilo.
“Tamasha hili ni kiunganishi muhimu kati ya wadau wa kahawa ambao hutoka sehemu mbalimbali na kupata fursa ya kubadilishana mawazo, lakini pia linatoa fursa kwa washiriki kupata elimu mpya ya uzalishaji wa zao hili pamoja na teknolojia mpya za ukaangaji na utayarishaji wa kahawa,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ubora na Uhamasishaji wa Masoko wa TCB, Frank Nyarusi, amesema jitihada za Serikali za kuweka mifumo thabiti ya usimamizi na huduma bora za ugani zimechochea ongezeko la bei ya kahawa, ubora na uzalishaji kwa wakulima nchini.
Amesema hivi sasa bei ya kahawa kwa mkulima imepanda maradufu ikilinganishwa na miaka minne iliyopita, hali inayowapa wakulima hamasa ya kuongeza ubora na uzalishaji.
“Kwa sasa mkulima anapata Sh12,000 kwa kilo moja ya kahawa ya Parchment (Arabika) ikilinganishwa na Sh4,000 hadi Sh5,000 zilizolipwa miaka minne iliyopita. Kwa upande wa kahawa ya Robusta, bei imepanda kutoka chini ya Sh1,500 hadi zaidi ya Sh5,000 kwa kilo moja,” amesema Nyarusi.
Amebainisha kuwa ongezeko hilo la bei limechochewa na mifumo ya kidijitali iliyowekwa na Serikali, ambayo imewezesha wanunuzi wengi kushiriki kwenye soko na kuongeza ushindani wa kibiashara.
Nyarusi amesisitiza kuwa ubora wa kahawa ndiyo unaouza bidhaa hiyo katika soko la dunia, hivyo akawataka wakulima kuendelea kuzingatia kanuni bora za kilimo.
Amesema uzalishaji wa kahawa nao umeimarika na kuongezeka kutoka wastani wa tani 60,000 hadi kufikia zaidi ya tani 80,000 kwa mwaka.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa kahawa, Julius Mollel ameomba itungwe sheria itakayowabana wakulima watakaong’oa miti ya kahawa bila kuwa na kibali maalumu, ili kuendeleza hadhi ya zao hilo ambalo ni alama ya mkoa huo.
“Kama mkulima, naomba wanasiasa wakifika bungeni watunge sheria ili kahawa itungwe sheria ya kuilinda kama nchi za wenzetu, kama mtu akitaka kung’oa kahawa apate kibali sahihi.
“Kama itabaki hivi, watu watajikatia tu, mwishoni mwa siku kahawa itapotea, wakati ‘icon’ ya Mkoa wa Kilimanjaro ni kahawa,” amesema mwenyekiti huyo.
Naye, Mwenyekiti wa tamasha hilo, Denis Mahulu, amesema linatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia Oktoba 3 hadi 5 mwaka huu, na litaenda sambamba na Siku ya Kahawa Duniani, ambayo huadhimishwa Oktoba mosi ya kila mwaka.