Wanachama 160 kutoka Mwanza kushuhudia Simba Day

MAKAMU Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Mkoa wa Mwanza, Juma Kayugwa amesema mashabiki na wanachama 54 wamewasili Dar es Salaam kwa ajili ya kushuhudia Tamasha la Simba Day litakalofanyika leo, Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kayugwa alisema wanatarajia kuwa na zaidi ya wanachama 160 kutoka Mwanza.

“Tumeambatana na baadhi ya viongozi wa matawi ya Mwanza na wanachama waandamizi kwa ajili ya Simba Day. Tumekuja kuungana na Wanasimba wenzetu kwa ajili ya tukio moja,” alisema Kayugwa na kuongeza.

“Tunaweza kufika zaidi ya watu 160. Tunatarajia kupata wageni zaidi kutoka Mwanza kwa sababu ni mkoa mkubwa. Kama viongozi tunafanya hamasa kubwa kuhakikisha lengo la timu kuujaza uwanja linatimia na imekuwa hivyo siku zote.”

Jumatano, Septemba 10, 2025, ni Simba Day, tamasha litakalofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, siku ambayo klabu hiyo hutambulisha wachezaji na benchi la ufundi kwa msimu mpya.