Babati. Watu wenye ulemavu 2,000 nchini watanufaika na pikipiki zenye magurudumu matatu zinazotumia nishati ya umeme, zinazotolewa bila malipo na taasisi ya Mati Foundation ya mjini Babati, mkoani Manyara.
Taasisi hiyo imeeleza mpango wake wa kutoa pikipiki hizo zaidi ya 2,000 kwa makundi ya watu maalumu ili kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika shughuli za utafutaji.
Kampuni ya Mati Super Brands Ltd, kupitia taasisi yake isiyo ya kiserikali Mati Foundation, imeanza rasmi mradi wa kukabidhi pikipiki za magurudumu matatu zinazotumia nishati ya umeme kwa watu wenye ulemavu nchini, ili kuwasaidia kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi zaidi.
Hafla ya makabidhiano imeongozwa na mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo inayozalisha na kusambaza vinywaji changamshi, David Mulokozi, leo Septemba 10 mwaka 2025 mjini Babati.
Mulokozi ameeleza kuwa watu wenye mahitaji maalumu katika jamii, hasa wale wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kuingiza kipato, wanahitaji kuwezeshwa kwa miundombinu bora ili wachangie uchumi wa Taifa kupitia kazi wanazozifanya.
“Tumekabidhi pikipiki kwa ajili ya ndugu zetu wenye ulemavu, hasa wale wanaofanya kazi, ili ziwasaidie katika shughuli zao na pia katika kujenga uchumi wa taifa letu,” ameeleza Mulokozi.
Baadhi ya wanufaika wa vyombo hivyo vya usafiri, wameishukuru taasisi hiyo kwa kugusa maisha ya jamii yenye makundi maalumu, wakieleza kuwa jitihada hizo zinakwenda kuleta chachu na kuongeza ufanisi katika shughuli zao.
Mkazi wa mtaa wa Wang’warayi, Ramadhani Omari, amesema, “Nimekuwa napoteza pesa na muda nikiwa nafuatilia madeni kwa ajili ya biashara yangu ya mahindi, sasa, kwa pikipiki hii itasaidia kufanya kazi zangu.’’
Mkazi wa mtaa wa Mji Mpya, ambaye naye amenufaika na pikipiki hizo, Aisha Wenga, ameshukuru kwa msaada huo kwani amepata nyenzo muhimu ya kumsaidia katika shughuli zake.
“Pikipiki hii itarahisisha shughuli zangu za kila siku katika kujitafutia riziki, tofauti na hapo awali,” amesema Wenga.
Meneja mradi wa Mati Foundation, Isack Piganio, amesema taasisi hiyo, ikishirikiana na Mati Super Brand, imekuwa ikijitolea kurudisha kwa jamii sehemu ya faida yake.
Piganio ameeleza kwamba mradi huo wa ugawaji wa pikipiki za magurudumu matatu umekuwa miongoni mwa miradi mingine ambayo wameendelea kuifanya.