ZEC yabaini jambo fomu za urais za Othman, ACT- Wazalendo yatoa msimamo

Unguja. Mtiania ya urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amepewa muda hadi  kesho, saa 3:00 asubuhi kukamilisha ujazaji wa fomu za kuomba uteuzi, baada ya kubainika kuwapo kwa kasoro.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetoa muda huo wa nyongeza kwa mujibu wa taratibu, ili kumpa fursa mtiania huyo kurekebisha dosari zilizobainika.

Wakati Othman akiendelea na mchakato wa kukamilisha fomu zake, mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Masoud Hamad, ameshindwa kupokelewa fomu zake kwa kushindwa kutimiza masharti yaliyowekwa na ZEC.

Pia, vyama vingine vitano vimeshindwa kurejesha fomu za kuomba uteuzi ambavyo ni SAU, CCK, UMD, UDP na DP. ZEC inatarajia kutangaza wagombea walioteuliwa leo, saa 11:00 jioni.

Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi, amesema leo, Septemba 10, 2025 uwa wamepokea fomu za mgombea wa ACT-Wazalendo kwa masharti, iwapo atashindwa kukamilisha mpaka muda aliopewa ataondolewa kwenye uteuzi.

“Tume imetoa muda mpaka kesho saa tatu asubuhi kazi hii ikamilike, ikifika muda huo bado masharti hayajatimizwa, hautateuliwa kugombea,” amesema Jaji Kazi.

Kwa mujibu wa sheria ya ZEC namba nne ya mwaka 2018, miongoni mwa masharti ya kujaza fomu za wagombea ni kuwa na wadhamini 200 kila mkoa kwa mikoa yote mitano ya Zanzibar wakiwa na kadi za wanachama husika na waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura.

Wakati Othman akirudisha fomu hiyo ilibainika kuwa mikoa miwili kati ya mitano fomu za chama hicho hazijasainiwa na wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya kwa kutokamilisha wadhamini kwenye mikoa ya Kaskazini Unguja na Kusini Unguja.

Akizungumzia changamoto hiyo, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Omar Said Shaaban, amesema walitimiza vigezo vyote vya kuwa na wadhamini wanachama wenye kadi, isipokuwa wasimamizi wa uchaguzi katika mikoa hiyo walikataa kuhakiki kadi hizo kupitia mfumo.

Amesema katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, wanachama 30 pekee walikuwa hawana kadi za gamba, lakini kadi zao zipo kwenye mfumo hivyo walitakiwa kuthibitishwa kupitia mfumo.

Baada ya maelezo kutoka upande wa ACT, baada ya muda Jaji amesema wamekubaliana kuzipokea, lakini wametoa muda wa kuhakiki wanachama hao mbele ya mkurugenzi wa uchaguzi ili kukamilisha idadi kisheria.

Hata hiyo leo jioni, chama hicho kilitoa taarifa kwa umma ikieleza kuwa kinaendelea na maandalizi ya uzinduzi wa kampeni, baada ya fomu za mgombea wao kupokelewa na ZEC.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa uzinduzi wa kampeni hizo utafanyika Pemba Septemba 13 na kisha Unguja Septemba 14.

“Othman Masoud Othman amerejesha fomu zake za uteuzi mbele ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na kupokelewa na Mwenyekiti, Jaji George Joseph Kazi.

“Wakati wa kuwasilisha fomu hizo, tume ilizipokea na kutoa barua ya kuthibitisha kupokea fomu hizo pamoja na maelekezo ya kuhakiki baadhi ya fomu za wadhamini jambo ambalo tayari tumelikamilisha bila ya kikwazo,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa Timu ya Ushindi, Ismail Jussa.

Kuhusu mgombea wa CUF, Jaji Kazi amesema ameshindwa kutimiza masharti kwa kutowasilisha fomu za mkoa mmoja wa Kaskazini Unguja, hivyo fomu zake hazikupokelewa.

Alipopewa muda wa kueleza kilichosababisha kutorejesha fomu hizo, Hamad amesema ni kutokana na changamoto ya mtandao tangu asubuhi, hivyo kushindwa kukamilisha kwa wakati.

Hata hivyo, Jaji Kazi amekataa sababu hiyo akisema walipewa muda mrefu wa kuchukua na kurejesha fomu tangu Agosti 30, kama kulikuwa na changamoto, alitakiwa aeleze tume kuona wanaitatuaje. Pia katika mfumo wa tume hakukuwa na changamoto hiyo.

Alipozungumza na waandishi wa habari nje ya chumba cha kupokea fomu, Hamad amesema anakubaliana na uamuzi wa tume, kwani kisheria hajatimiza vigezo.