ACT yafanikiwa kuhakiki majina wadhamini wa mgombea urais, ZEC yathibitisha

Unguja. Chama cha ACT Wazalendo kimefanikiwa kukamilisha uhakiki wa wadhamini wa mgombea kiti cha urais wa Zanzibar, Othman Masoud kama kilivyoelekezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi.

Licha ya fomu za mgombea huyo kupokewa jana Septemba 10, 2025 fomu za mikoa miwili ya Kaskazini Unguja na Kusini Unguja majina ya wadhamini hayakuthibitishwa na maofisa wa uchaguzi wa wilaya kutokana na kutokuwa na kadi halisi za wanachama.

Hata hivyo, Mwanasheria mkuu wa chama hicho, Omar Said Shaaban alisema sio kwamba walikosa wadhamini badala yake wasimamizi wa uchaguzi walikataa kupokea taarifa za wanachama hao kupitia kwenye mfumo, kwani kadi zao zilikuwa za kielektroniki.

Kutokana na changamoto hizo, Jaji Kazi alimuagiza Mkurugenzi   ZEC, Thabit Idarous Faina na mwanasheria mkuu wa chama hicho wakae na kuhakiki taarifa hizo na ziwe zimekamilika hadi kufikia leo Septemba 11, 2025 saa 3:00 asubuhi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Septemba 11, 2025 ofisini kwake, Faina amesema wamefanikiwa kuhakiki taarifa hizo na kutimiza vigezo vya mgombea kuwa na wadhamini 200 kila mkoa kama takwa la kisheria linavyoelekeza.

Amesema maofisa wa Tehama wa ACT Wazalendo na wa ZEC walikutana mapema leo na kuzipitia fomu hizo na kukamilisha taratibu kama ilivyoelekezwa.

“Kwa mkoa wa Kaskazini Unguja jumla ya wanachama 250 waliorodheshwa kuwa wadhamini, hata hivyo katika uthibitisho uliofanywa jumla ya wanachama 11 waligundulika taarifa zao hazikuwa sahihi, kwa vile nambari za kadi za wanachama hao hazikuendana na majina yao.”

“Kwa Mkoa wa Kusini Unguja jumla ya wanachama 207 waliorodheshwa kuwa wadhamini hata hivyo katika uthibitisho huo, wanachama sita waligundulika taarifa zao hazikuwa sahihi kwa vile nambari za kadi za wanachama hazikuendana na majimbo.”

Hata hivyo, amesema kwa sasa kinachosubiriwa ni kufanya uteuzi ambao unatarajiwa kufanyika leo saa 11:00 jioni.

Katika taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa timu ya ushindi ya chama hicho, Ismail Jussa imesema wamekamilisha kazi ya uhakiki na wanaendelea na maandalizi ya uzinduzi wa kampeni.

“Tunaendelea na maandalizi ya uzinduzi wa kampeni utakaofanyika Septemba 13, 2025 kisiwani Pemba.”