Rorya. Watu sita wamefariki dunia papo hapo na mmoja kujeruhiwa baada ya gari walikokuwa wakisafiria kugonga kwa nyuma gari lililokuwa limeegeshwa barabarani baada ya kuharibika.
Ajali hiyo imetokea katika Kijiji cha Buganjo wilayani Rorya wakati gari aina ya Toyota Succeed likiwa limebeba watu saba likiwa linatoka mjini Tarime kuelekea Kijiji cha Busurwa wilayani Rorya, liligonga kwa nyuma gari aina ya Fuso liliokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara baada ya kuharibika..
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Mark Njera ameeleza ajali hiyo imetokea leo Septemba 11,2025 saa 11 alfajiri.
“Gari aina ya Succeed iliyokuwa inatoka Tarime kuelekea Rorya iligonga kwa nyuma gari aina ya Fuso lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara baada ya kuharibika,” amesema
Amesema majina ya watu hao hayajatambulika na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Utegi wilayani Rorya huku hali ya majeruhi ikiwa ni mbaya.
Amesema Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wamedai chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa madereva wote wawili ambapo wa Fuso aliegesha gari bila kuweka alama ya tahadhari.
“Huyu dereva wa gari dogo naye inaonekana alikuwa mwendo kasi hakuchukua tahadhari na mbaya zaidi amehama upande wake kwenda wa pili sasa ile anashtuka tayari ameparamia Fuso,” amesema Bernard Okos.
Amewaomba madereva kuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka athari za ajali zinazoweza kuzuilika.
Godfrey Godfrey amedai watu hao ni wafanyabiashara wa dagaa na walikuwa wakielekea kwenye shughuli zao katika mwalo wa Busurwa wilayani Rorya.