AKILI ZA KIJIWENI: Benni McCarthy asiitumie Tanzania kujitetea Kenya

MARA mbili tofauti, Benni McCarthy ameizungumzia timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika mazingira ambayo hata hakukuwa na sababu za kuitaja au kuizungumzia hadi kijiwe kikamshangaa.

Ya kwanza ilikuwa ni baada ya kumalizika kwa hatua ya makundi ya mashindano ya CHAN 2024 ambapo katika mazungumzo yake na waandishi wa habari akasema Tanzania iliyokuwa imeongoza kundi B ndio itajua aina ya kundi ambalo Kenya ilikuwepo kwa vile itakutana na Morocco.

McCarthy aliamini Taifa Stars ilikuwa kundi jepesi na Kenya yake ilikuwa kundi gumu lakini jambo la kushangaza, timu ambayo ilishika nafasi ya pili kwenye kundi la Taifa Stars ikaitoa Kenya ambayo ilikuwa ni Madagascar na Tanzania tukatolewa na Morocco ambayo baadaye ilitwaa ubingwa.

Juzi tena baada ya Kenya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 akasema anatamani kuwepo na shindano maalum la kirafiki ambalo litahusisha timu za Kenya na Tanzania zicheze ili kuamua timu gani mshindi na anatamani vilivyo kuionyesha umwamba Taifa Stars.

Baada ya tathmini ya kijiwe, tumebaini kwamba Benni McCarthy tunatakiwa tumpotezee tu na wala tusiingie katika mtego wake kwa kutaka kumjibu kila anachokiongea kuhusu Tanzania.

Anachokifanya McCarthy ni kutaka kuitumia Taifa Stars kama njia ya kutafuta huruma kwa Wakenya baada ya timu hiyo kukosa muelekeo katika kuwania kufuzu Kombe la Dunia na pia kukwamia robo fainali kwenye mashindano ya CHAN 2024.

Inaonekana amegundua kwamba Wakenya wana ushindani fulani hivi dhidi ya Tanzania hivyo pengine anapotuponda angalau inasaidia kupunguza presha upande wake na kufurahisha waajiri wake ambao wana maswali mengi ya kumuuliza kuhusu mwenendo wa timu hiyo.

Na tusiingie katika mtego wa mechi ya kirafiki na Kenya maana sisi tuko juu katika chati ya ubora wa FIFA kuliko wao ambapo sisi tupo nafasi ya 103 na wao wako katika nafasi ya 109.

Kama tukicheza hiyo mechi, tukapata shindi, hatuwezi kupanda sana katika viwango vya ubora ila tukifungwa au kutoka sare, sisi tutaporomoka na wao watapanda zaidi.