Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Shinyanga imefuta hukumu ya kifungo cha miezi sita jela alichohukumiwa Pendo Elikana, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kuwa aliombwa amuue Luhaga Mpina.
Mpina amekuwa mbunge wa Kisesa kwa vipindi vitatu (2005–2020) kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Pendo alishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu katika kesi ya jinai namba 9605/2025 kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma, akatiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela bila kuwapo chaguo la kulipa faini.
Mrufani (mshtakiwa), katika utetezi, alidai kupokea simu kwa njia ya WhatsApp kutoka kwa shahidi wa pili wa Jamhuri, aliyetajwa kwa jina moja la Musa, akiomba msaada wa kumuua Luhaga Mpina na akiahidiwa kulipwa fedha.
Hakuridhishwa na hukumu na adhabu hiyo, hivyo akakata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga. Rufaa imesikilizwa na Jaji John Kahyoza aliyetoa hukumu jana, Septemba 10, 2025, akifuta hukumu ya awali na kumwachia huru mrufani.
Katika hukumu ambayo nakala imepakiwa kwenye mtandao wa mahakama, Jaji amesema kutiwa hatiani kwa mshtakiwa (mrufani) hakukuwa kwa haki, hivyo amebatilisha kutiwa kwake hatiani, adhabu aliyopewa na kumwachia huru.
Kupitia wakili Kilatu, Pendo alipinga hukumu akiwa na sababu nane. Wakati wa usikilizwaji rufaa aliondoa sababu ya saba na ya nane, huku ya 1, 2, 3 na 5 aliziwasilisha kwa pamoja na ya sita akaiwalisha pekee.
Katika sababu ya kwanza, alidai hakimu alikosea kisheria kumtia hatiani na kumhukumu kwa kuegemea ushahidi ambao haukujitosheleza, kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindishwa kuthibitisha shitaka hilo pasipo kuacha shaka.
Pia alidai hakimu alikosea kumpa adhabu kubwa bila faini, wakati kosa aliloshtakiwa nalo lina adhabu mbadala ya faini, ikizingatiwa kuwa mrufani alikuwa mkosaji wa mara ya kwanza, tena mwenye umri wa miaka 19.
Wakili wa Serikali, Francisca, alipinga rufaa akidai upande wa mashtaka ulithibitisha shtaka pasipo kuacha shaka, hivyo hitimisho la Mahakama lilikuwa sahihi.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji alisema kuna hoja mbili zinazotakiwa kuamuliwa na Mahakama ambazo ni iwapo upande wa mashtaka ulithibitisha kosa la kutoa taarifa za uongo kwa mtu ambaye ameajiriwa katika utumishi wa umma, na pili, ni kama adhabu aliyopewa ilikuwa sahihi kisheria.
Wakili wa mrufani alidai upande wa mashtaka ulishindwa kuchunguza au kufafanua kuwa simu kwa njia ya WhatsApp haikutumika kama njia ya mawasiliano, licha ya mrufani kusisitiza mawasiliano hayo yalikuwa kwa njia hiyo.
Upande wa mashtaka uliegemea ushahidi wa shahidi wa kwanza aliyeandika maelezo ya mrufani, huku shahidi wa nne akithibitisha hakuna mawasiliano kati ya mrufani na shahidi wa pili katika tarehe inayodaiwa.
Shahidi wa pili alikana kuwasiliana na mrufani, huku upande wa mashtaka ukieleza mawasiliano yalikuwa kwa njia ya WhatsApp ila hayakutolewa kwa polisi.
Jaji amesema, baada ya kukagua rekodi, anaona Mahakama ya chini ilikubali ushahidi wa shahidi wa kwanza hadi wa nne kama mashahidi wa kuaminika.
Hata hivyo, amesema mlalamikaji hakutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai ya mawasiliano ya WhatsApp.
Jaji Kahyoza amesema mrufani katika utetezi wake alidai kupokea simu ya WhatsApp kutoka kwa shahidi wa pili wa Jamhuri katika kesi hiyo.
“Ni sawa, kama ilivyowasilishwa na upande wa mashtaka, kwamba mrufani alitaja WhatsApp katika utetezi wake, hata hivyo, taarifa yake ya awali kwa polisi haionyeshi kwamba Musa aliwasiliana naye kupitia WhatsApp,” amesema na kuongeza:
“Zaidi ya hayo, wakili wa upande wa utetezi hakumhoji shahidi yeyote wa upande wa mashtaka iwapo uchunguzi ulihusisha uwezekano wa simu ya WhatsApp kati ya mrufani na Musa.”
Jaji amesema, muhimu zaidi, upande wa mashtaka ulikuwa na wajibu wa kuthibitisha pasipo shaka yoyote madai ya mrufani, kwamba Musa alimpigia simu akimwomba amuue Luhaga Mpina, ni habari za uongo.
Amesema upande wa mashtaka ulitoa vielelezo viwili ambavyo ni Know Your Customer (KYC) na CDR kutoka kwa mtoa huduma (Hallotel) ili kuthibitisha kwamba hapakuwa na simu ya kawaida kati ya mrufani na Musa katika tarehe iliyodaiwa.
“Hata hivyo, hawakuchunguza iwapo Musa aliwasiliana na mrufani kupitia WhatsApp, kama alivyodai,” amesema.
Jaji amesema anaona upande wa mashtaka haukupinga uwezekano wa mawasiliano kwa njia ya WhatsApp, kwa hiyo, ulishindwa kubaini kuwa maelezo ya mrufani yalikuwa ya uongo.
“Katika mazingira hayo, upande wa mashtaka haukuthibitisha kosa pasipo kuacha shaka yoyote. Kutokana na hayo, hukumu inafutwa. Mrufani aachiwe huru isipokuwa kama ameshikiliwa vinginevyo kihalali,” ameamuru jaji.
Iwapo hukumu ilikuwa halali, amesema: “Baada ya kuweka kando hukumu hiyo, ningependa kusema maneno machache kuhusu hukumu hiyo.”
Jaji Kahyoza amesema mrufani alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miezi sita, ambacho ni cha juu zaidi kwa kosa hilo, licha ya kwamba kosa chini ya kifungu cha 122(b) cha Kanuni ya Adhabu kinatoa faini mbadala ya Sh100,000.
“Alikuwa mkosaji wa mara ya kwanza, mwenye umri wa miaka 19, bila rekodi yoyote ya awali. Miongozo ya hukumu (katika ukurasa wa 33) inaelekeza kwamba hukumu za kifungo zinapaswa kuwa hatua ya mwisho, hasa pale ambapo sheria inatoa njia mbadala na mkosaji ni mkosaji wa mara ya kwanza,” amesema.
“Katika kesi ya sasa, hakimu hakuonyesha kuzingatia sababu hizi za kupunguza adhabu, wala kueleza kwa nini chaguo la faini lilikataliwa. Kwa mtazamo wangu, kutolewa hukumu ya kifungo katika hali hiyo ilikuwa ni matumizi yasiyofaa ya busara,” amesema na kuongeza:
“Mbaya zaidi, Mahakama ilitoa adhabu ya juu zaidi kwa kosa ambalo mrufani alitiwa hatiani bila kupuuza ukweli kwamba mrufani alikuwa mkosaji wa mara ya kwanza.”
Amesema, katika kesi hiyo, hakuna sababu za kuridhisha zilizoainishwa ili kutoa adhabu ya juu zaidi, kwa hiyo adhabu ilikuwa ya kupindukia.
Amehitimisha kuwa kifungu cha 122(b) cha Kanuni ya Adhabu kinatoa fursa ya kulipa faini na kuwa, Bunge limetoa fursa ya kulipa faini au kifungo, Mahakama inapotoa adhabu, ihakikishe adhabu ya faini inapaswa kutolewa kwanza, na kushindwa kulipa faini hiyo, basi hukumu ya kifungo inaweza kutolewa.