Unguja. Wakati ikizinduliwa sera ya nishati, imetajwa kukuza uwekezaji katika utafiti, teknolojia na uvumbuzi kwenye maeneo ya nishati safi, matumizi bora na teknolojia za kisasa zinazopunguza gharama na kuongeza ufanisi.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 11, 2025 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi wakati wa kuzindua sera hiyo Unguja Zanzibar.
Amesema sera hiyo inahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kupunguza moshi na kemikali hatarishi zinazotokana na matumizi ya kuni, mkaa na mafuta machafu hatua hiyo itapunguza magonjwa ya mfumo wa kupumua na matatizo mengine ya kiafya.
“Serikali imeweka dhamira ya dhati ya kuijenga Zanzibar yenye uchumi shindani, kijani na jumuishi kuhakikisha nishati ya uhakika inaendelea kuimarika nchini kwani sekta hii ndio injini ya maendeleo ya viwanda, utalii, kilimo cha kisasa, teknolojia ya habari na maisha ya kila mwananchi,” amesema.
Dk Mwinyi amesema sera hiyo itawawezesha wanawake kwani mara nyingi wanahusika na shughuli za kupika, kwani matumizi ya nishati safi inawapa nafasi zaidi ya kushiriki katika shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.
Dk Mwinyi amesema lengo la sera hiyo ni kuhakikisha upatikanaji wa nishati nafuu na ya uhakika kwa wananchi wote, kuongeza usalama wa nishati kupitia vyanzo vya ndani na usambazaji wa aina mbalimbali za nishati.
Pia, ni kuendeleza matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira kwa kuhamasisha uzalishaji wa umeme wa jua, upepo, biofuel na gesi, nyuklia na kushirikisha sekta binafsi kupitia uwekezaji na ubia.
Akizungumzia mpango mkuu wa umeme wa Zanzibar 2025/50, amesema umeandaliwa kwa mara ya kwanza nchini ukiwa na lengo la kutoa picha ya utabiri wa mahitaji ya umeme ya Zanzibar hadi mwaka 2050.
Kupitia mpango huo, upatikanaji wa taarifa zinazohusiana na mahitaji ya umeme Unguja na Pemba utakuwa rahisi kufikia mwaka 2050.
“Kwa msingi huo, miradi mikubwa ya kuzalisha nishati itaendelezwa, ikiwemo ya nishati ya jua, upepo, mitambo ya gesi na mifumo ya akiba ya umeme kupitia teknolojia za ‘battery storage’,” amesema.
Mbali na hayo, amesema matarajio ya utekelezaji wa sera hiyo na mpango mkuu wa umeme Zanzibar ni kuongeza upatikanaji wa umeme kwa jamii hasa maeneo ya vijijini na yasiyo na umeme wa uhakika.
Amesema pia kuweka mkazo katika matumizi ya vyanzo vya nishati safi kama vile nishati ya jua na upepo na kuendeleza miundombinu ya umeme ikiwemo mitambo ya kuzalisha umeme, usambazaji na mifumo ya akiba ya umeme.
Sambamba na hayo, amesema ni kuimarisha mifumo ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya nishati ili kuhakikisha ufanisi na uwazi katika shughuli za nishati na kuchangia maendeleo ya uchumi wa buluu kwa kutumia nishati endelevu na kuimarisha mazingira.
Matarajio mengine amesema ni kuweka mikakati ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa nishati safi na ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi kwa kuvutia wawezekaji kupitia sera rafiki na mazingira bora ya biashara.
Amesema matarajio hayo yanatarajiwa kuimarisha maisha ya wananchi, kuchochea maendeleo ya kiuchumi, na kulinda mazingira, hivyo kuchangia kufikia uchumi wa kipato cha kati na cha juu ifikapo mwaka 2050.
Ametumia fursa hiyo kuwataka viongozi na taasisi zote zilizoguswa katika utekelezaji wa sera hiyo kushirikiana pamoja na Wizara ya Maji, Nishati na Madini ili kufanikisha utekelezaji wa malengo ya sera hiyo na kuimarisha ustawi wa maendeleo endelevu ya Zanzibar.
Rais Mwinyi amewapongeza washirika wa maendeleo wa kikanda na kimataifa likiwamo Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA), Benki ya Dunia kwa msaada wao katika kuendeleza jitihada mbalimbali za sekta hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kilangi amesema sera hiyo inalenga kuhakikisha Zanzibar inakuwa na huduma ya nishati ya uhakika, endelevu na salama ili kuendana na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kilangi amesema kupitia sera hiyo, Zanzibar imetoa kipaumbele juu ya ujenzi na matumizi ya miundombinu imara ya nishati inayoweza kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi na mikakati ya dharura, ili kuhakikisha huduma ya nishati inaendelea kupatikana bila kukatika.
Naye mtaalamu mwandamizi wa Nishati kutoka Benki ya Dunia, Dk Rhonda Jordan Antoine amesema benki hiyo ni mshirika wa karibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mkakati wa benki hiyo wenye thamani inayokaribia dola milioni 400 sawa na Sh997.2 bilioni, unaotekelezwa katika maeneo ya maendeleo ya miji, nishati, elimu, utalii na ustahimilivu.