DK.SAMIA: UWT KWA MARA YA KWANZA IMETOA MGOMBEA URAIS,TWENDENI TUKASAKE KURA


Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Urambo

KWA mara ya kwanza Jumuiya ya Umoja Wanawake Tanzania(UWT) kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) imetoa mgombea Urais hivyo waende kusaka kura za mgombea wao kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Hayo yamesema na Mgombea Urais kupitia CCM Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara wa kampeni kwa ajili ya kuomba ridhaa kwa wananchi wa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora.

Amesisitiza kwamba kwa mara ya kwanza Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kupitia CCM umetoa mgombea Urais.”Kwa mara ya kwanza katika nchi yetu miaka yote wagombea Urais wanatokea jumuiya ya umoja wa vijana na jumuiya ya wazazi.

“Maana yake wanaume wanakuwa umoja wa vijana mpaka umoja wa wazazi.UWT haikuwahi kutoa mgombea Urais, huu ni mwaka wa kwanza ni mara ya kwanza kwa UWT kutoa mgombea Urais kwanini nasema hivyo?

“Kinamama muungane kuanzia sasa, kitenge kiunoni na kiatu mguuni twende tukasake kura za mgombea wetu wa Urais.Tukamweke mgombea wetu wa Urais mwanamke, twendeni tukasake kura za mgombea wetu.”

Awali akizungumza na wananchi wa Urambo waliojitokeza maelfu kwa maelfu kuhudhuria mkutano huo wa kampeni zake za kugombea Urais ,Dk.Samia ametumia nafasi hiyo kumshukuru mgombea ubunge wa Jimbo la Urambo Magreth Sitta kwani alimpokea bungeni na kumlea na ndio amemfungulia njia.

“Urambo mimi ni nyumbani kwasababu mama Magreth Sitta amenipokea katika Bunge la 10 tukiwa mabinti wadogo, alinilea kwa miaka mitano. Marehemu Kaka yangu Mzee Samuel Sitta alinilea vyema katika Bunge la Katiba na kule ndiko ulipoonekana uwezo wangu katika siasa. Kwa hiyo niko katika jimbo la nyumbani.”