Tanzania, kama mataifa mengi yanayoendelea, imewekeza pakubwa katika elimu ya juu kupitia vyuo vikuu vyake. Hivi ni vituo vya maarifa, utafiti na uvumbuzi, vikiwa na jukumu la kuzalisha wataalamu na suluhisho kwa changamoto za jamii. Lakini swali linasalia: Je, ubunifu unaozalishwa unaweza kubadilishwa kuwa fursa za kiuchumi?
Kwa muda mrefu, vyuo vikuu vimejikita zaidi katika kufundisha na kufanya tafiti za kimsingi, matokeo yakibaki kwenye majarida ya kisayansi badala ya kuchangia moja kwa moja uchumi. Lakini katika karne ya sasa ambapo teknolojia na ubunifu ni nguzo za maendeleo, dhana hii inahitaji kubadilishwa.
Nchi zilizoendelea zimeonyesha vyuo vikuu kuwa injini za ukuaji wa uchumi kupitia ubunifu wa kibiashara. Mfano wa Silicon Valley na ushirikiano wake na Stanford au UC Berkeley ni kielelezo tosha.
Tanzania pia ina uwezo. Vyuo vikuu vyake vina watafiti wenye vipaji, wanafunzi makini, na miundombinu ya maabara. Kila mwaka miradi mingi ya utafiti hufanyika katika afya, kilimo, uhandisi na TEHAMA. Changamoto kubwa ni ukosefu wa mifumo ya kuhamisha teknolojia (technology transfer). Vyuo vingi havina ofisi maalumu zenye wataalamu wa masoko, sheria za miliki bunifu na maendeleo ya biashara. Watafiti wengi hawajui kulinda ubunifu wao au kuupeleka sokoni, hivyo fursa hupotea.
Utamaduni wa kitaaluma pia ni changamoto. Watafiti hutunukiwa zaidi kwa machapisho ya kisayansi kuliko uvumbuzi unaoweza kuzalisha biashara. Mfumo huu wa tathmini unakwamisha motisha ya kubadili tafiti kuwa biashara. Mabadiliko yanahitajika ili vyuo vitambue na kuunga mkono jitihada za kibiashara.
Uhusiano dhaifu kati ya vyuo vikuu na sekta binafsi pia ni tatizo. Sekta binafsi ingeweza kutoa mitaji, masoko na uzoefu, huku vyuo vikuu vikitoa suluhisho bunifu kwa changamoto zao. Mfumo huu wa ushirikiano, maarufu kama triple helix (serikali, sekta binafsi na vyuo vikuu), ni muhimu kwa uvumbuzi endelevu. Hata hivyo, nchini Tanzania, ushirikiano huu bado ni dhaifu; makampuni hayafahamu tafiti za vyuo vikuu na vyuo havielewi mahitaji ya sekta binafsi.
Ili kufanikisha ujasiriamali wa kisayansi, hatua kadhaa ni muhimu. Kwanza, vyuo vikuu viimarishe ofisi za uhamishaji teknolojia (TTOs) zenye wataalamu wa kisheria, masoko na biashara. Ofisi hizi zitasaidia kulinda miliki bunifu, kutafuta wawekezaji na kuandaa mipango ya biashara.
Pili, serikali iongeze uwekezaji katika utafiti na maendeleo na kuweka sera zinazohamasisha ubunifu. Inaweza kutoa ruzuku kwa miradi ya kibiashara, mikopo nafuu kwa wajasiriamali wa vyuo vikuu na motisha za kodi kwa kampuni zinazoshirikiana navyo.
Tatu, mitaala ijumuishe masomo ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara na miliki bunifu. Hii itawawezesha wanafunzi na watafiti kugeuza mawazo kuwa biashara. Aidha, vyuo vihamasishe kuanzishwa kwa start-ups na spin-offs.
Nne, vyuo vikuu viimarishe mahusiano na sekta binafsi kupitia mikutano ya mara kwa mara, maonyesho ya ubunifu na majukwaa ya ushirikiano.
Mwisho, jamii pia inapaswa kuthamini na kutumia bidhaa na huduma zinazozaliwa kutokana na tafiti za ndani.
Kwa ujumla, vyuo vikuu vya Tanzania vina nafasi kubwa kuchangia sio tu maarifa bali pia uchumi wa taifa. Kwa kuwekeza katika mifumo, kubadili mitazamo na kuimarisha ushirikiano, tafiti za vyuo vikuu zinaweza kubadilika kutoka kwenye karatasi na kuwa chanzo cha ajira na mapato. Ni wakati sasa kuona utafiti ukiongoza si tu kwenye maarifa, bali pia kwenye faida halisi za kiuchumi.