Kazi ipo nusu fainali ligi ya Kikapu Dar

UTAMU wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) umehamia katika nusu fainali ya ligi hiyo. Inaonyesha kila mchezo utakaochezwa utakuwa ni kama fainali.

Hiyo imetokana na uwezo mkubwa ulioonyeshwa na timu hizo katika ligi hiyo, na ugumu wa nusu fainali utakaotokea ni kutokana na kila timu kuhitaji kushinda ili iweze kucheza fainali.

Timu hizo ni Dar City, Stein Warriors, JKT na Pazi, na upande wa wanawake ni Jeshi Stars, JKT Stars, DB Troncatti na DB Lioness.

Nusu fainali upande wa wanaume itachezwa kati ya timu ya Dar City na Stein Warriors, JKT na Pazi.

Timu ya Dar City ilitinga nusu fainali baada ya kuifunga Srelio katika michezo 2-0, huku timu ya Stein Warriors ikiifunga UDSM Outsiders michezo 2-0.

Katika robo fainali nyingine, JKT iliifunga Savio kwa michezo 2-0, huku Pazi ikiifunga ABC katika michezo 2-1.

Timu hizo ziliwahi kukutana katika hatua ya mzunguko ambapo Dar City iliishinda Stein Warriors kwa pointi 70-60 na Pazi ikaifunga JKT kwa pointi 63-50.

Kwa upande wa wanawake, itakuwa ni kati ya timu ya Jeshi Stars na DB Troncatti, na Jeshi Stars na DB Lioness.

Karabani Karabani, kocha mkuu wa timu ya Stein Warriors, amesema mipango yao waliyojiwekea ni kuhakikisha wanacheza mashindano ya kufuzu kucheza Ligi ya Ubingwa wa Afrika (BAL).

Timu ya Stein Warriors inashiriki ligi hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kupanda daraja mwaka jana pamoja na timu za Kurasini Heat na Polisi.

Katika nusu fainali ya ligi hiyo, timu ya Dar City itakuwa na nyota wake wote ambao ni Sharon Ikedigwe, Amin Mkosa, Ally Abdallah, Clinton Best, Fotius Ngaiza na Jamal Marbuary.

Kwa upande wa timu kongwe ya Pazi itakuwa na Soro Geofrey, Josephat Peter, Robert Tasire na Victor Michael.

Stein Warriors itakuwa na Jonas Mushi, Brian Mramba, Sisco Ngaiza na Evance Davies, huku timu ya JKT ikiwa na Baraka Sabibi, Isakwisa Mwamsope, Jackson Brown na Omary Sadiki.

Kwa upande wa JKT Stars itakuwa na Jesca Ngisaise, Sara Budodi, Grance Innocent na Wade Jaha.

Kamishina wa Ufundi na Mashindano wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), Haleluya Kavalambi, amesema tarehe ya mchezo wa nusu fainali itatangazwa baada ya Mashindano ya Majeshi (BAMATA) kuisha Zanzibar.