Dodoma/Dar. Mgombea urais wa Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina ameshinda kesi dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuhusu shauri la maombi ya Kikatiba akipinga kuenguliwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mpina alienguliwa katika kinyang’anyiro hicho na INEC Agosti 26, 2025, hivyo pamoja na Bodi ya Wadhamini ya ACT-Wazalendo alifungua kesi dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Agosti 27, 2025.
Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma katika uamuzi iliyoutoa leo Septemba 11, 2025 imesema INEC ilimuengua Mpina katika mchakato huo isivyo halali kwa kuwa haikumpa haki ya kumsikiliza.
ACT-Wazalendo ilifungua kesi kutokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wa Mpina kuomba kuteuliwa na INEC kuwa mgombea urais na INEC kumzuia kurejesha fomu ya kuomba kuteuliwa.
Katika shauri hilo namba 21692 la mwaka 2025 lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, chama hicho pamoja na mambo mengine kilipinga uamuzi wa INEC kumwengua Mpina katika orodha ya wagombea walioomba kuteuliwa.
Badala yake kinaiomba Mahakama iielekeze INEC ipokee fomu ya mgombea huyo kwa ajili ya uhakiki na uteuzi.
Shauri hilo lilisikilizwa na majaji, Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa na John Kahyoza, kwa njia ya maandishi.
Mahakama ilihitimisha usikilizwaji huo Septemba 8, 2025 baada ya mawakili wa pande zote kufafanua baadhi ya hoja zao za maandishi na mahakama ikapanga kutoa uamuzi leo Septemba 11.
Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo, Agosti 6, 2025 kuomba uteuzi wa INEC kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025
Hata hivyo Agosti 26, Msajili wa Vyama vya Siasa, alitangaza kubatilisha uteuzi wake kutokana na pingamizi lililowasilishwa kwake na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala aliyedai uteuzi wa Mpina ni batili, hakuwa na sifa kwa mujibu Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa Chama, Toleo la mwaka 2015.
Wajibu maombi kupitia jopo la mawakili wa Serikali lililoongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo lilipinga madai na hoja za waombaji, pamoja na mambo mengine wakidai INEC haikuwa na sababu ya kuwasikiliza kulingana na uharaka wa mchakato huo.
Mahakama katika uamuzi imeamuru INEC ipokee fomu zake za kuomba utezi na iendelee na mchakato wa uteuzi kuanzia ulipokuwa umeishia.
Katika kufikia uamuzi huo, Mahakama ilizingatia mambo matatu yaliyohitaji majibu ambayo ni iwapo INEC ilifanya uamuzi wa kumuengua Mpina kwa maelekezo au amri ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kama waombaji hawakupewa haki ya kusikilizwa na afua gani zitolewe kwa wadaawa.
Katika uamuzi uliosomwa na Jaji Kagomba, Mahakama imekataa kuwa INEC iliamua hivyo kwa maelekezo au amri ya Msajili.
Hata hivyo, imekubali kuwa uamuzi wa INEC kuzuia kurejeshwa fomu za uteuzi Agosti 27, 2025 bila kupewa haki ya kusikilizwa ulikuwa unakinzana na Ibara ya 13(6) (a) ya Katiba ya nchi.
Ibara hiyo inaelekeza mtu kusikilizwa kwa ukamilifu kuhusu jambo linalofanyiwa uamuzi na chombo chohcote dhidi yake.
Jaji Kagomba amesema kitendo cha INEC cha Agosti 26, 2025 kuandika barua kuwazuia waombaji kuwasilisha fomu za uteuzi kilifanywa bila kuwa na mamlaka kamili kwa sababu muda wa kuwazuia ulikuwa haujafika.
Amesema kwa kuwa waombaji walizuiwa bila kusikilizwa, uamuzi huo unapaswa kufutwa kama ilivyoelezwa katika uamuzi wa kesi mbalimbali na Mahakama ya Rufaa.
Kuhusu afua gani zitolewe kwa wadaawa, Mahakama imesema kwa kuzingatia kuwa haki za waombaji zimekiukwa inatoa afua kuwa:
Chini ya Ibara ya 74 (11) ya Katiba, INEC ni chombo huru na hakiwajibiki kufuata amri ya mtu yeyote au ya taasisi yoyote ya Serikali ikiwamo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Pia, imetamka kwamba, INEC ilifanya uamuzi ambao umewaathiri waombaji na kwamba, iliwanyima fursa ya kuwasikiliza, hivyo barua ya INEC ya Agosti 26, 2025, (kuwazuia waombaji kuwasilisha fomu) ni kinyume cha Katiba na haina nguvu yoyote kisheria.
“Baada ya kutamka hivyo, tunatamka kwamba waleta maombi wapewe fursa haraka iwezekanavyo ya kuwasilisha fomu za mleta maombi wa pili (Mpina) na mchakato wa kuzipokea uendelee ulipoishia Agosti 27, 2025,” amesema Jaji Kagomba.
Vilevile, Mahakama imesema kwa kuwa shauri hilo ni kwa ajili ya kuongeza uelewa wa haki kwa umma, gharama za shauri zitabebwa na kila upande.
Pia, imekataa maombi ya waombaji ya kulipwa fidia ya Sh100 milioni ikisema inaona kwa mazingira ya kesi hiyo amri hiyo si mahala pake.
Wakili Fulgence Massawe, amesema kwa uamuzi huo wa Mahakama sasa Mpina ataingia kwenye kampeni za uchaguzi mkuu.
Amesema ingawa kampeni zilishaanza takribani wiki mbili sasa, kama alikuwa amejipanga pamoja na chama chake kwa rasilimali bado atafanya vizuri.
Amesema Mpina akiingia kwenye kinyang’anyiro hicho atachangamsha hata kampeni zinazoendelea kwa kuwa kati ya wagombea wa upinzani yeye ndiye mwenye kuleta ushindani kwa mgombea wa CCM, kulingana na umaarufu wake na hoja zake ambazo amekuwa akiziibua
Akizungumza baada ya hukumu, Mpina amesema haki imetendeka na sasa anakwenda kushinda uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Amesema suala la kuchelewa siyo shida kwake bali hata kama zingebaki siku 15 bado alikuwa na uhakika wa kwenda kushinda uchaguzi.
Kampeni za uchaguzi mkuu zilianza Agosti 28 na zitahitimishwa Oktoba 28, 2025.
Amewataka wagombea wengine wasitafute huruma ya Mahakama katika kusaka kura.
“Baada ya hukumu hii sasa niko tayari, namsikiliza Katibu wangu awasiliane na tume wakitupangia hata sasa hivi niko tayari kuzipeleka ili nianze harakati za kusaka kura, waache twende kwenye ballot paper (boksi la kura)” amesema.
Zitto Kabwe, kiongozi mstaa wa chama hicho amesema huu si wakati wa maneno mengi, badala yake wanataka kupata muda wa kusaka ushindi wakati kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu akisema haki imetendeka.
Mmoja wa machifu waliomsindikiza Mpina mahakamani, Josephat Nkingwa (Chifu Kisendi II) amesema wameshuhudia haki ikitendeka mahakamani.
Chifu Kisendi II ambaye ni Mwenyekiti wa Machifu Kanda ya Usukumani, amesema mara zote vyombo vya uamuzi vinapojipambanua na kusimama kwa haki vinakuwa na heshima.