Kocha mkuu wa Yanga, Romain Folz amesema wachezaji wà timu wapo tayari kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kesho dhidi ya Bandari Kenya, aliosema utakuwa na mvuto wa aina yake, huku akiitaja Simba.
Yanga inatarajiwa kuhitimisha kilele cha Wiki ya Mwananchi kesho kwa kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Bandari Kenya.
Hilo ni pambano la saba kwa msimu wa matamasha ya Yanga yaliyoanza rasmi mwaka 2019.
Folz amesema ameandaa kikosi hicho kwa muda mrefu kuhakikisha kinafanya vema katika mechi hiyo pamoja na ile wa Ngao ya Jamii itakayopigwa Septemba 16 dhidi ya Simba.
Amesema ukubwa wa tamasha hilo utadhihirisha jinsi Yanga ilivyo kubwa Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya mashabiki.
“Wachezaji wapo vizuri isipokuwa mmoja tu, ambaye ni majeruhi licha ya kuwa ni mara yangu ya kwanza kuwepo katika Kilele cha Wiki ya Mwananchi, naamini nitawapa burudani mashabiki wetu,” amesema Folz na kuongeza;
“Wachezaji wapo tayari na wataonyesha mchezo mzuri kutokana na maandalizi tuliyoyafanya naomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuishuhudia timu yao ikionyesha mpira mzuri na wa ushindani.”
Folz amesema, licha ya ugeni katika kikosi hicho ana matumaini makubwa ya kuwa na kikosi kizuri kutokana na aina ya wachezaji alionao ambao amekiri kuwa wapi tayari huu ni mwanzo na ni kipimo sahihi kuelekea mchezo wa dabi Septemba 16.
Yanga kabla ya mchezo huo imecheza mechi dhidi ya Yanga U20, Rayon Sport, Fountain Gate, Tabora United na dhidi ya JKT Tanzania mechi zote waliibuka na ushindi.