Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Jimbo la Mbagala kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Saidi Kinyogoli ameahidi kuanzisha Saccos maalumu kwa ajili ya kutoa mikopo kwa kina mama, pamoja na kuanzisha kituo cha maendeleo na kuboresha miundombinu ya jimbo hilo, endapo atachaguliwa kuwa mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza leo, Septemba 11, 2025, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za CUF katika Viwanja vya Zakhem, Kinyogoli amesema kuwa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni msingi wa maendeleo endelevu katika jamii.
“Tutahakikisha kina mama wanapata mikopo kupitia Saccos tutakazozianzisha, ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuchangia katika maendeleo ya familia na Taifa,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa moja ya kipaumbele chake ni kuboresha sekta ya afya kwa kuandaa semina maalumu kwa wahudumu wa afya, wakiwemo wa Hospitali ya Zakhem, ili kuongeza weledi na kuondoa vitendo vya manyanyaso kwa wagonjwa.
“Kwa sasa huduma za afya Mbagala zinakabiliwa na changamoto kubwa, hasa ukosefu wa utu na vitendo vya manyanyaso vinavyofanywa na baadhi ya wahudumu. Hali hii inawakatisha tamaa wagonjwa na lazima ishughulikiwe,” amesisitiza Kinyogoli.
Mgombea huyo ameahidi kuwa sauti ya wananchi bungeni kwa kushirikiana nao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili Jimbo la Mbagala.
“Huduma zetu hospitalini zimekuwa kero, wajawazito wanalala watatu kwa pamoja katika kitanda kimoja, wagonjwa wanasukumwa mateke na wengine wananyimwa huduma kwa sababu tu ya ukali wa wahudumu,” amesema Kinyogoli na kuongeza kuwa;
“Nikichaguliwa, hatua ya kwanza nitakayochukua ni kuandaa semina za mara kwa mara kwa wauguzi na madaktari wote wa Jimbo la Mbagala. Lengo ni kuwakumbusha wajibu wao na kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa utu na heshima.”

Mgombea ubunge wa CUF jimbo la Mbagala, Said Nyogoli akiwatambulisha wagombea udiwani wa chama hicho kwa jimbo hilo.
Kuhusu changamoto za kiuchumi, Kinyogoli amesema akinamama wa Mbagala wamekuwa wakihadaiwa na mikopo yenye riba kubwa na mingine kutowafikia kabisa, licha ya kuchangishwa fedha za kuanzisha akaunti.
“Tutaunda Saccoss za akinamama zitakazosaidia kuendesha biashara ndogo ndogo bila kuingia kwenye mikopo ya kausha damu. Mikopo itakayotolewa itakuwa na masharti nafuu na riba isiyozidi asilimia 10, ili mama zetu waweze kusimama kimaisha bila kunyanyasika,” amesema Kinyogoli.
Aidha, amesema atafungua kituo maalumu cha vijana kwa ajili ya kutoa elimu juu ya fursa za maendeleo na namna ya kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu iliyopo na itakayotekelezwa jimboni.
“Vijana wanahitaji eneo la kujifunza na kushiriki katika miradi ya maendeleo. Kituo hiki kitawawezesha kupata uelewa juu ya barabara, huduma za maji, elimu, michezo na hata mbinu za kujiendeleza kimaisha kupitia ajira zitakazojitokeza kutokana na miradi ya Serikali,” amesema.
Amesema yeye si mwanasiasa wa maneno bali vitendo hivyo anaomba kura ili kuondoa machozi ya kina mama, kuwapa vijana mwanga wa maisha na atahakikisha huduma za afya zinakuwa za kibinadamu.
Naye, mjumbe wa kamati ya kampeni, Ally Mohamed, maarufu Kadogoo amesema leo wananchi wa Mbagala wanahoji kama kweli wapinzani pekee ndio waliokoma, au maisha magumu yamewakumba wote bila kujali chama.
Kadogoo amesema bei ya mafuta imepanda, huduma za afya hazipatikani, na hata mama wa kawaida anajikuta akiuza mihogo barabarani bila uhakika wa mteja.
Amesema hali ya maisha imekuwa ngumu kiasi kwamba familia nyingi hazichagui tena chakula wanachotaka, bali wanakula tu kile kinachopatikana. Wananchi wanasema sasa imekuwa kawaida kula utumbo, ngozi au miguu ya kuku badala ya nyama, huku vijana wakikosa ajira na akinamama wakisaga maisha kwa kuuza mazao mitaani.
“Wanawake wetu wamechoka, sura zimekauka, na umaskini umewabana kiasi kwamba haijulikani nani ni mrembo tena,” amesema Kadogoo.
Wakazi wa Mbagala wanasema adui yao mkubwa si wapinzani bali umaskini unaosababishwa na maamuzi ya viongozi walioko madarakani. Wameeleza kuwa wanasiasa wamejiongezea marupurupu na mafao makubwa ya kustaafu, wakati wananchi wa kawaida wakibaki kula pilipili na mihogo.