Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto amewaita mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mbinu bora za kocha Romain Folz na ubora wa nyota wapya.
Mwamnyeto amefunguka hayo mbele ya wanahabari akisisitiza, wapo tayari kutoa burudani kwa mashabiki ambao watajitokeza Uwanja wa Mkapa, huku akiweka wazi tayari wameingia katika mfumo wa kocha huyo.
“Licha ya kwamba kocha ni mpya ndani ya timu tayari tumeshaelewa mifumo yake lakini wachezaji wapya ambao wamesajiliwa dirisha lililofungwa hivi karibuni na wao tayari tumetengeneza muunganiko bora,” amesema Mwamnyeto na kuongeza;
“Nawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia kikosi chao bora kilichobeba matumaini msimu huu ambao malengo yetu ni kuwa timu bora na shindani.
“Ubora wa mbinu bora za Folz utaonekana kwenye uwanja wa Mkapa, kesho njooni kwa wingi mshuhudie mbinu sahihi za kocha wetu ambaye ana malengo makubwa na timu hii.”
Mwamnyeto amesema kwa upande wao kama wachezaji wapo tayari kwa ushindani na wamejiandaa vizuri kutoa burudani nzuri uwanjani.