Mwijage amkosha Maximo Kagame | Mwanaspoti

MIONGONI mwa wachezaji ambao kocha wa KMC, Marcio Máximo anavutiwa na uwezo wao kwenye kikosi hicho ni pamoja na Edson Erick Mwijage ambaye amepachika mabao mawili na kutoa asisti mbili katika mashindano ya Kombe la Cecafa Kagame.

Mwijage ambaye ni usajili mpya wa KMC akitokea Kagare Sugar ambayo ilishuka daraja msimu uliopita, amehusika katika mabao manne kati ya matano yaliyofungwa na timu hiyo katika hatua ya makundi.

Maximo alisema mchango wa Mwijage umeleta uwiano mkubwa ndani ya kikosi, hasa kwenye sehemu ya ushambuliaji ambako KMC imekuwa na changamoto kwa muda mrefu.

“Tunahitaji kuwa bora zaidi katika eneo la mwisho, nafurahia kuwa na wachezaji kama Mwijage, anaonyesha kuwa na kitu na amekuwa akijituma. Hii ndiyo sababu anaendelea kufanya vizuri kwenye mashindano haya kwa kushirikiana na wenzake,” alisema Maximo.

Kocha huyo raia wa Brazil aliongeza kuwa, uwezo wa mchezaji huyo wa kujiweka kwenye nafasi sahihi na kufanya uamuzi wa haraka umezidi kumpa imani huku akiamini anaweza kupata kilicho bora pia kutoka kwa wachezaji wengine kwenye kikosi hicho.

“Nilipomuona mara ya kwanza nilijua ana kitu cha tofauti kama ilivyo kwa wachezaji wengine. Ameonyesha ujasiri dhidi ya wapinzani wakubwa na hilo ndilo linalotufanya tuwe na matumaini naye,” alisema kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa.

KMC sasa inajiandaa kuvaana na Singida Black Stars katika hatua ya nusu fainali ya Kagame, mchezo utakaopigwa Jumamosi, baada ya mabadiliko ya ratiba.

Maximo amesema anajua mchezo huo hautakuwa rahisi, lakini anaamini mchango wa wachezaji wake unaweza kutoa tofauti kubwa uwanjani.

“Tunaiheshimu Singida, ni timu nzuri iliyo na wachezaji wenye ubora. Lakini tukiwa na nidhamu ya kiufundi na kujituma, naamini tuna nafasi ya kufanya kitu,” alisema.

Katika hatua ya makundi, Singida BS ambayo ilimaliza kinara wa kundi A ikiwa na pointi saba, imefunga mabao matatu na kuruhusu moja, hivyo ina wastani wa kufunga kwenye kila mchezo.