Bunda. Mgombea urais wa Chama cha Chaumma, Salum Mwalimu ameahidi kufufua kilimo cha pamba na kukiunganisha moja kwa moja na viwanda, ili kuongeza thamani ya zao hilo na kuwanufaisha wakulima, endapo atachaguliwa kuongoza dola katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Akizungumza leo, Septemba 11, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Stendi ya zamani, Bunda Mjini, Mwalimu amesema kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuinua uchumi wa wananchi kupitia matumizi bora ya rasilimali zilizopo, hususan katika sekta ya kilimo na viwanda.
Amesema mvuto wa kilimo cha pamba umepungua kutokana na ukosefu wa mipango madhubuti na sera thabiti kama zile zilizokuwepo enzi ambapo kilimo na uzalishaji wa viwandani vilikuwa vinapewa kipaumbele.
“Tumerithi mfumo uliodhoofisha sekta ya kilimo kwa kuikosa dira na msukumo wa viwanda. Tunahitaji kuhuisha sera, kuwekeza katika viwanda vya kuchakata pamba, na kuhakikisha wakulima wananufaika moja kwa moja na jasho lao,” amesema Mwalimu mbele ya mamia ya wakazi wa Bunda waliohudhuria mkutano huo.

Mgombea huyo ameongeza kuwa dhamira yake ni kuondoa umaskini kwa Watanzania kupitia uchumi wa viwanda unaojengwa juu ya kilimo chenye tija, huku akisisitiza usimamizi mzuri wa rasilimali na uwekezaji unaozingatia masilahi ya wananchi.
“Nikichaguliwa kuwa rais, nitakwenda kuwa kiongozi wa watu. Tutakifufua kilimo cha zao la pamba na kukiunganisha na viwanda ili kuondokana na umaskini wa kipato. Uwezo huo ninao, kikubwa ni mipango na dhamira ya kweli,” amesema Mwalimu.
Mwalimu amesema tatizo lingine ni kutokuwepo kwa mazingira rafiki ya uzalishaji, masoko ya uhakika, pamoja na miundombinu ya kuchakata mazao ya pamba, kumepelekea wakulima wengi kugeukia mazao mengine yenye faida ya haraka na soko la uhakika.
” Hali hii inaleta changamoto kubwa kwa juhudi za kufufua sekta ya pamba ambayo kwa muda mrefu ilikuwa uti wa mgongo wa uchumi wa maeneo mengi ya vijijini.”
“Ili kurejesha hamasa ya wakulima, kuna haja ya Serikali na wadau husika kurejea upya katika kupanga sera na mikakati yenye kuimarisha mnyororo mzima wa thamani wa zao hili muhimu. Ndicho Chaumma tutakifanya,” amesema Mwalimu.
Mbali na pamba, Mwalimu ameahidi pia kufufua kiwanda cha kusindika minofu ya samaki kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kutengeneza ajira kwa vijana wa maeneo hayo.
“Ziwa lipo, samaki wapo, lakini kiwanda kimekufa. Tutarudisha uhai wa viwanda hivi ili vijana wetu wanufaike na rasilimali za kwao badala ya mataifa ya nje kunufaika kwa kusafirisha bidhaa ghafi kutoka kwetu,” amesisitiza.
Akiendelea kunadi sera zake, Mwalimu alikosoa chama tawala akidai kimeshindwa kutumia rasilimali za Taifa kuinua uchumi na maisha ya wananchi.
Amesema fikra mpya za uongozi zinahitajika ili kurejesha dira ya maendeleo aliyokuwa nayo hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Bunda Mjini kupitia Chaumma, Mwira Mwira ameahidi kupigania upatikanaji wa stendi ya kisasa kwa ajili ya wakazi wa mji huo, akieleza kuwa iliyopo kwa sasa haikidhi mahitaji ya wananchi na inakuwa kero kubwa wakati wa mvua.
“Haiwezekani wananchi wanaendelea kuteseka, hakuna choo, hakuna miundombinu mizuri. Nipeni kura, niwakilishe kwa hoja zenye nguvu kwenye vikao vya halmashauri,” amesema Mwira.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chaumma, John Mrema amewataka wananchi wa Bunda kutumia nafasi yao kuleta mabadiliko kwa kuchagua viongozi jasiri, wenye dira na uthubutu wa kupigania masilahi ya wananchi.
“Ni wakati wenu sasa. Msipoteze fursa hii. Oktoba 29 hakikisheni mnafanya uamuzi wa kihistoria,” amesema Mrema.
Baada ya mkutano mkuu, Mwalimu alihitimisha mikutano yake ya siku tatu ya kunadi sera mkoani Mara na kuanzia kesho anatarajiwa kuingia mkoani Simiyu kuendelea na kushawishi umma kumchagua.