SIMBA juzi ilihitimisha shangwe la Simba Day msimu wa 17 kwa kuwapa raha Wanamsimbazi kwa burundani ya wasanii mbalimbali pamoja na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, huku baadhi ya nyota wa timu hiyo wakiwa hawaamini walichokiona Kwa Mkapa.
Katika tamasha hilo lililopambwa na burudani mbalimbali ikiwamo ya muziki na mechi za timu za klabu hiyo ikiwamo ile iliyofungia hesabu kwa Mnyama kuendeleza ubabe kwa kuwanyoa K’Ogalo, kuna baadhi ya nyota waling’ara na kuwa gumzo, lakini wenyewe wakishangaa nyomi waliloliona.
Tamasha la Simba Day, limekuwa likibeba mambo mengi ambapo huwa kuna shughuli za kijamii zinafanyika, kisha kilele chake ndipo burudani hutolewa huku safari hii Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ukilipokea tamasha hilo kwa aina yake kupitia burudani za muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali na mechi ya kirafiki Simba ikicheza dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
Ukiachana na ushindi wa mabao 2-0 ilioupata Simba katika mchezo huo wa kirafiki kupitia mabao ya Abdulrazack Hamza dakika ya 6 na Steven Mukwala dakika ya 48, Mwanaspoti linakuletea matukio yaliyobamba zaidi.
Siku mbili kabla ya tamasha, Simba ilitangaza tiketi zote zimeisha, hiyo ilimaanisha mashabiki wamelipokea kwa mikono miwili.
Ilipofika siku ya tukio, mashabiki walifika uwanjani mapema na kuibua vaibu la kutosha. Saa mbili kabla ya kuanza kwa utambulisho wa wachezaji, hali ya Uwanja wa Benjamin ilikuwa inapendeza kwa rangi nyekundu na nyeupe kutokana na viti vingi kukaliwa na mashabiki wa Simba waliokuwa wakishangilia matukio yote yaliyokuwa yakiendelea.

Katika shoo za wasanii zilizofanywa, ile ya mwisho kutoka kwa mtumbuizaji mkuu, Mbosso ilibeba hisia za wengi huku kila mmoja akionekana kuridhishwa na alichofanya.
Mbosso ambaye ni msanii wa Bongo Fleva, aliingia uwanjani saa 11:02 jioni na kupiga shoo ya nguvu akiimba nyimbo zaidi ya 15 zikiwemo Sele, Kunguru, Moyo, Yataniua, Shetani, Ova, Haijakaa Sawa, Amepotea, Nusu Saa, Pawa, Aviola na Asumani.
Shoo hiyo ya Mbosso iliyodumu kwa takribani saa 1, ilimalizika saa 12:05 jioni, iliwaacha mashabiki na furaha iliyopitiliza, huku kubwa zaidi ni madansa alioingia nao ukiwa ni msafara mkubwa.
Kabla ya Mbosso, walifanya shoo wasanii mbalimbali akiwemo Joh Makini na Chino ambao nao waliteka kijiji.

Hapa kulikuwa na balaa la aina yake, mashabiki waliofika uwanjani walikuwa na hamu kubwa sana kuyaona majembe yao mapya kwa msimu wa 2025-2026.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alikuwa na jukumu la kutambulisha kikosi ambapo alianza jukumu hilo saa saa 12:21 jioni kwa kulitambulisha benchi la ufundi lililoongozwa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.
Baada ya hapo, wakafuata wachezaji wakiwemo 13 wapya ambao ni Yakoub Suleiman, Antony Mligo, Naby Camara, Rushine De Reuck, Vedastus Masinde, Wilson Nangu, Alassane Kante, Morice Abraham, Hussein Daud Semfuko, Mohamed Bajaber, Neo Maema, Seleman Mwalimu na Jonathan Sowah.
Wengine ni vijana watatu waliopandishwa kutoka Simba U20 ambao ni Alexander Erasto, Hussein Mbegu na Bashir Salum.

Kocha wa Simba akizungumza kwa niaba ya benchi la ufundi alisema msimu huu wamejipanga na utakuwa na mafanikio makubwa ikiwamo kutwaa makombe na kufanya makubwa kuliko msimu uliopita, huku Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji, akiahidi atafurahi kuona tuzo ya Afrika inakuja Tanzania kupitia Simba na anaamini hilo linawezekana msimu huu.
GOR MAHIA YAIPA PA KUANZIA
Baada ya matukio yote hayo kufanyika, ilifuatia mechi ya kirafiki ya kimataifa ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Katika mchezo huo, Fadlu alianza na kikosi chenye mchanganyiko wa wachezaji wapya na wa zamani. Kikosi kilikuwa hivi; Moussa Camara, Ladack Chasambi, Antony Mlingo, Rushine De Reuck, Chamou Karaboue, Abdulrazack Hamza, Kibu Denis, Naby Camara, Neo Maema, Jean Charles Ahoua na Jonathan Sowah.

Mechi hiyo ilipomalizika, mashabiki na hata Fadlu, wametoa maoni yao, kuna maeneo bado hayajakaa sawa na yanahitaji kufanyiwa maboresho haraka kabla ya kufika Septemba 16, 2025, siku ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.
Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza dhidi ya Gor Mahia, Fadlu alianza na wachezaji watano wapya, jambo ambalo liliwafanya mashabiki wa Simba kuwafuatilia kwa makini na kuona vile wanaweza kuwa msaada katika kikosi chao kuelekea msimu ujao.
Miongoni mwa wachezaji hao ambao walionekana kufanya vizuri zaidi ni pamoja na Rushine De Reuck na Naby Camara ambao walitumika kwa dakika nyingi zaidi ukilinganisha na wachezaji wengine.
Rushine ambaye alianza kucheza sambamba na Chamou Karaboue kwenye eneo la beki ya kati kisha, Abdulrazack Mohamed Hamza, alionekana kuwa na utulivu mkubwa hasa katika kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma.

Ni beki mwenye matumizi mazuri ya akili, alikuwa kikwazo kwa Gor Mahia kwa kufanya tackling mbili wakati ambao Simba ilikuwa ikishambuliwa huku akipiga mipira miwili mirefu kutokea nyuma katika kipindi cha pili na mmoja ulichangia upatikanaji wa bao la Mukwala huku asisti ikitolewa Ladack Chasambi.
Nyota mwingine mpya ambaye alifanya vizuri zaidi ni Naby Camara ambaye alianza kama kiungo wa kati, alionekana kuelewa kwa haraka staili ya ucheza ya Simba kwa kuwa chachu ya timu kusogea mbele kwa haraka huku akishirikiana vizuri na Charles Jean Ahoua na Neo Maema.
Mbali na hao, Antony Mligo naye alifanya vizuri dakika 45 za kipindi cha kwanza kabla ya kufanyiwa mabadiliko.
Simba ilipofanya mabadiliko kipindi cha pili, Fadlu aliamua kumtumia Naby upande wa beki ya kushoto ambako napo aliendelea kufanya vizuri kwa upande wa Jonathan Sowah na Maema wanaonekana bado wanahitaji muda zaidi kuendelea kutazamwa.
Kwa upande wa wachezaji wengine wapya ambao waliingia walionekana kuwa na kitu licha ya muda mchache ambao walipata, kipa Yakoub Suleiman ndiye aliyefanya vizuri zaidi kwa wachezaji ambao waliingia, alichukua nafasi ya Moussa Camara, aliokoa mchomo mmoja wa hatari katika kipindi cha pili kabla naye kufanyiwa mabadiliko.
Naby, Rushine na Sowah wameongelea vile ambavyo wameshangazwa na mapokezi yao katika tamasha hilo.
Naby alisema; “Nimepokelewa kwa heshima kubwa na mashabiki wa Simba, imenipa nguvu ya kupambana zaidi. Najua bado nina kazi kubwa ya kuonyesha, lakini nimefurahi kuona mashabiki wananikubali mapema.”
Rushine ambaye ni raia wa Afrika Kusini naye alisema: “Sikuwa natarajia mapokezi makubwa kiasi hiki. Nilipoingia uwanjani nilihisi kama nimecheza hapa muda mrefu kwa sababu mashabiki walinipa moyo. Najua Simba ni klabu kubwa na kila mchezaji anapaswa kujituma kwa kiwango cha juu. Nitahakikisha ninakuwa msaada mkubwa kwa timu hii.”

Kwa upande wake Sowah alisema: ”Ni jambo kubwa kwangu kuvaa jezi ya Simba na kusimama mbele ya mashabiki wengi namna hii. Mapokezi niliyopata yamenipa hamasa kubwa. Najua kadiri muda unavyosonga nitaonyesha makali yangu tukutane msimu ujao.”
Kwa ushindi huo, Simba imeendelea kuwa na wakati mzuri katika Tamasha la Simba Day tangu 2009 na sasa imeshinda michezo 12 ya kirafiki.
Katika historia ya michezo ya Simba Day kuanzia mwaka 2009 hadi sasa 2025, Simba imeshinda dhidi ya SC Villa (2009, 2013 na 2015), AFC Leopards (2016), Rayon Sports (2017), Asante Kotoko (2018), Power Dynamos (2019 na 2023), Vital’O (2020), St George (2022), APR (2024) na Gor Mahia (2025).
Pia imetoa sare moja pekee dhidi ya Express mwaka 2010, huku ikipoteza michezo minne dhidi ya Victors (2011), Nairobi City Stars (2012), Zesco United (2014) na TP Mazembe (2021).