Takukuru yaonya vitisho, upendeleo na ununuzi wa kura siku ya uchaguzi

Geita. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita imewataka wasimamizi wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, kuhakikisha mchakato huo unafanyika katika mazingira salama, yenye haki, bila ununuzi wa kura, vitisho wala upendeleo.

Akizungumza leo, Septemba 11, 2025, wakati wa semina ya maofisa uchaguzi ngazi ya jimbo na wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata kwa majimbo ya Geita Mji na Geita, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, James Ruge, amesema wasimamizi hao wanapaswa kusimamia kwa uadilifu na kushughulikia malalamiko yote ya uchaguzi kwa uwazi.

“Ni jukumu lenu kuhakikisha hakuna vitisho, hakuna ununuzi wa kura na hakuna upendeleo siku ya kupiga kura. Baada ya kura kupigwa, msimamie kwa uwazi na mshughulikie malalamiko kwa haki,” amesema Ruge.


Ameongeza kuwa mwaka huu ni muhimu kwa wananchi kwani wanatumia kura zao kuamua mustakabali wa haki na maendeleo yao, lakini rushwa inaweza kuathiri mchakato huo.

“Kura inayohusishwa na rushwa inaondoa sifa ya uchaguzi huru na haki, na inapoteza imani ya wananchi,” amesema Ruge.

Ruge amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha mapambano dhidi ya rushwa yanaendelea, na kwamba mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wasimamizi wa uchaguzi kuelimisha jamii juu ya madhara ya rushwa na namna ya kuzuia mianya yake.

Kwa upande wake, ofisa kutoka Takukuru aliyewasilisha mada ya sheria ya uchaguzi, Said Lipunjaje, amewataka wasimamizi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kuepuka kusababisha matokeo kubatilishwa.

“Ukifanya makosa utashtakiwa. Kwa mfano, ni kosa kughushi au kufuta daftari la mpigakura. Kifungu cha 120 cha Sheria ya Uchaguzi kinazuia mwenendo usiofaa kwa wasimamizi,” amesema Lipunjaje.


Ofisa Uchaguzi wa Jimbo la Geita, Sarah Yohana, amewataka wasimamizi kusimamia maadili ya uchaguzi kwa uwazi, bila upendeleo wa chama wala mgombea yeyote.

“Muwe waangalifu kubaini mapema vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani kwa lengo la kuvuruga uchaguzi,” ameongeza Yohana.

Naye Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata, Mpanduji Charles, amesema wako tayari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kanuni ili uchaguzi uwe huru na wa haki.