WAKATI Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) ikifikia hatua ya nusu fainali, inaonyesha timu ya Tausi Royals na Dar City ndizo zilizofanya ushindani wa ligi hiyo uongezeke.
Ushindani huo umetokana na usajili mzuri uliofanywa na timu hizo na kufanya timu nyingine ziongeze jitihada zaidi.
Hata hivyo, licha ya timu ya Tausi Royals kutolewa katika hatua ya robo fainali, inaonyesha haikuwa na bahati ya kusonga mbele.
Timu ya Tausi Royals, iliyoanzishwa mwaka jana na Gerald Gulaka na kushiriki Ligi ya WBDL mwaka huo, ilitolewa katika robo fainali na JKT Stars kwa michezo 2-1, na mwaka huu ikatolewa na DB Troncatti kwa michezo 2-1.
Kuwepo kwa timu ya Tausi Royals katika Ligi ya WBDL kulifanya timu nyingine zijipange zaidi kuhakikisha hazipotezi mchezo dhidi ya timu hiyo ngeni.
Timu nyingine ni Dar City, iliyoanzishwa na Mussa Mzenji. Ushindani wake ulitokana na usajili wa nyota wa kimataifa.
Usajili huo ulifanya wachezaji wa timu nyingine waongeze jitihada zaidi kuhakikisha hawatoi nafasi kwa wachezaji wa kigeni kutawala.
Wachezaji hao ni Sharon Ikedigwe, Clinton Best (Nigeria), Jamal Marbuary (Marekani), Victor Mwoka (Kenya), na wazawa ambao ni Amin Mkosa na Ally Abdallah.