Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili wafanyabiashara sita wakiwemo wamiliki wa jengo lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, umekamilika.
Kwa sasa upande wa Jamhuri upo katika hatua ya kuchapa nyaraka muhimu zilizopo katika jalada hilo ili washtakiwa hao wasomewa Maelezo ya mashahidi na vielelezo, kisha kesi hiyo ihamishiwe Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Alhamisi Septemba 11, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa katika kesi hiyo ambao wote ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni Leondela Mdete(49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam(61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour(38) mkazi wa Ilala.
Wengine ni Soster Nziku(55) mkazi wa Mbezi Beach, Aloyce Sangawe(59) mkazi wa Sinza na Stephen Nziku(28) mkazi wa Mbezi Beach.
Kato ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi umekamilika na tupo katika hatua ya uchapaji wa jalada ili ihamishiwe Mahakama Kuu,” amesema Kato na kuongeza
“Kutokana na hilo, tunaiomba Mahakama yako itupatie wiki moja ili tuweze kumalizia taratibu za uchapaji ili kesi iweze kuendelea na hatua nyingine ikiwemo kuihamishia Mahakama Kuu.”
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo hayo, alikubaliana na upande wa mashtaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, 2025 kwa ajili ya kutajwa na kama watakuwa wamekamilisha uchapaji, siku hiyo watawasomewa washtakiwa hao maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022,
Kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, washtakiwa hao isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Said Juma.
Katika shitaka la pili hadi la 31, washtakiwa hao siku na eneo hilo wanadaiwa kusabisha kifo cha Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Catherine Mbilinyi.
Vile vile, wanadaiwa kusababisha kifo cha Elton Ndyamukama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuph, Ally Ally, Ajuae Lyambiro, Mary Lema na Khatolo Juma.
Walisababisha pia, kifo cha Sabas Swai, Pascal Ndunguru, Brighette Mbembela, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Pascalia Kadiri, Issa Issa, Lulu Sanga, Happyness Malya na Brown Kadovera.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 29, 2024 na kusomewa mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia katika kesi ya mauaji namba 33633/2024.