Musoma. Wakazi wa vijiji 136 vinavyozunguka bonde la Mto Mara katika wilaya sita mkoani humo, wanatarajiwa kupata mafunzo kuhusu uhifadhi endelevu wa bonde hilo hatua ambayo inalenga kupunguza shughuli za binadamu zinazofanywa katika bonde la mto huo zinazohatarisha uhai wake.
Mbali na elimu pia zaidi ya miti 8,000 inatarajiwa kupandwa katika maeneo mbalimbali yanayozunguka bonde hilo ili kulinusuru na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Alhamisi Septemba 11,2025, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema shughuli hizo zitafanyika ikiwa ni sehemu maadhimisho ya 14 ya mto Mara yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 12 hadi 15 mwaka huu kwa kushirikisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Kanali Mtambi amesema uamuzi wa kutoa elimu kwa wakazi hao unatokana na kuwepo kwa shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya hifadhi ya bonde hilo muhimu kwa ustawi wa jamii na utalii katika nchi hizo tatu.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma juu ya maadhimisho ya 14 ya siku ya Mara yanayotarajiwa kuanza Septemba 12,2025 wilayani Butiama. Picha na Beldina Nyakeke
“Kuna shughuli nyingi zinafanyika wakati wa maadhimisho ya Mto Mara ikiwa ni pamoja na upandaji wa miti, tumebaini vitu hivi vinaharibika kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo ukosefu wa elimu kwa hiyo tunatumia siku nne hizi pamoja na mambo mengine kutoa elimu kwa wananchi hawa, ili wajue kuwa wana wajibu wa kushiriki kikamilifu kwenye utunzaji bonde hili,” amesema.
Kanali Mtambi amesema kutokana na umuhimu wa bonde la mto huo suala la elimu ya uhifadhi litakuwa endelevu ili kutoa msukumo mkubwa kwa hifadhi ya mto huo.
Amesema katika maadhimisho hayo pia kutakuwa na kongamano la kisayansi ambapo mada mbalimbali zitatolewa kuhusiana na uhifadhi endelevu kutoka kwa watafiti wa ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wamesema suala la uhifadhi wa bonde la mto Mara linahitaji ushirikiano kati ya jamii, Serikali na wadau wengine ili kupata matokeo chanya.
“Nimefurahi kusikia wanakwenda vijijini kutoa elimu hii kwa wananchi ambapo itawasaidia kuona wana jukumu la kuhakikisha mto Mara unakuwa salama muda wote,” amesema Joan Samo.
Amesema kwa muda mrefu kumekuwepo na utekelezaji wa shughuli mbalimbali hasa upandaji wa miti katika hifadhi hiyo lakini miti hiyo inakosa uendelevu wake, kutokana na kuharibiwa na binadamu au kukosa uangalizi wa karibu.
Machela Pius amesema baada ya elimu kutolewa hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wanaokwenda kinyume na sheria ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira hususan katika vyanzo vya maji.
“Sheria inasema shughuli za kibinadamu zifanyike nje ya mita 60 kutoka kwenye chanzo lakini wapo watu wanafanya shughuli zao ndani ya mita tano ingawa kutokujua sheria sio utetezi, lakini kwa vile watakuwa wamepata elimu kinachofuata sheria ichukue mkondo wake,” amesema.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Dk Masinde Bwire amesema bonde la Mto Mara lina mchango mkubwa katika ustawi wa Ziwa Victoria kwa ujumla na maandalizi ya maadhimisho hayo ya 14 yamekamilika.
Amesema pamoja na uwepo wa maadhimisho hayo bado kuna changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira katika bonde hilo unaotokana na matumizi mabaya ya ardhi ikiwepo ukataji miti hovyo, malisho na kilimo katika eneo hilo.
Amesema bonde la Mto Mara ni daraja la ikolojia ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa upande wa Tanzania na ile ya Maasai Mara kwa upande wa Kenya, hivyo lisipohifadhiwa vizuri kuna hatari ya kukosekana kwa faida zinazotokana na utalii kwenye hifadhi hizo.
Maadhimisho ya siku ya Mara hufanyika kila Septemba 12 hadi 15 kufuatia uamuzi wa baraza la mawaziri wa kisekta wanaouhusika na bonde la ziwa Victoria kwa nchi za Afrika Mashariki, yakiwa na lengo la kutoa msukumo mkubwa kwa uhifadhi wa bonde la mto Mara kwa ajili ya uendelevu wa bonde la Ziwa Victoria.