Wakili afungua kesi akiomba wafungwa kupata unyumba gerezani

Dar es Salaam. Wakili mkoani Iringa amewasilisha ombi Mahakama Kuu akiomba itamke kuwa, vifungu vya sheria vinavyowazuia wafungwa kuonana faragha na wenza wao wa ndoa na kupata unyumba havina uhalali Kikatiba.

Vilevile, ameiomba Mahakama itoe amri kwamba, wafungwa walio katika ndoa halali waruhusiwe kukutana faragha na wenza wao kinyumba bila usimamizi wa askari magereza.

Katika kesi aliyofungua Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Iringa, wakili Geofrey Mwakasege anadai kutokuwapo vifungu katika Sheria ya Magereza na Kanuni za Uendeshaji wa Magereza za mwaka 1968 vinavyoruhusu mwanandoa kuonana faragha na kupata unyumba na mwenza wake aliye gerezani ni kinyume cha Ibara ya 16(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Jeshi la Magereza Tanzania, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye pia ni mshauri mkuu wa kisheria wa Serikali.

Anadai zuio hilo kwa wanandoa halina masilahi ya umma na linakiuka haki ya faragha inayohusu haki za ndoa kama zilivyoainishwa katika Ibara ya 16(1) ya Katiba.

Ibara ya 16(1) ya Katiba inasema: “Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi.”

“Wakati jamii na Serikali zikihimiza wanandoa kuepuka talaka na kuimarisha familia, ambazo ndizo taasisi kuu za jamii, hakuna sababu wala mantiki kwa nini mwanandoa asiruhusiwe kuonana faragha kinyumba na mwenza wake aliye gerezani,” amedai.

Amedai Kanuni za Magereza zinaruhusu mazungumzo na wageni gerezani kwa sharti kwamba yafanyike mbele ya macho ya askari.

Mwakasege anadai kizuizi hicho ni kinyume cha Sheria ya Ndoa na haki za mtu aliye katika ndoa, huku kikihimiza talaka pale mmoja anapohukumiwa kifungo. Anadai pia ni kinyume cha mila na desturi za Kitanzania.

Amedai haki ya unyumba ni msingi wa kuimarisha uhusiano wa wanandoa, hivyo kuwakosesha wafungwa waliohukumiwa haki hiyo kunawanyima wanandoa nafasi ya kuendeleza uhusiano wao wa kifamilia.

“Ukosefu wa haki ya unyumba unaweza kusababisha wafungwa kuendelea kurudia tabia za kihalifu, kwa kuwa ustawi wa kihisia na kisaikolojia wa mfungwa unategemea uhusiano wake na familia,” amedai.

Amedai tatizo hilo si la wafungwa pekee, bali linaathiri pia wenza wao, familia na jamii kwa jumla.

“Zuio la haki ya unyumba linasababisha mateso ya kihisia yasiyo ya lazima, talaka na misukosuko ya kifamilia, hivyo kudhoofisha malengo ya urekebishaji na urejeaji wa wafungwa katika jamii,” amedai.

Amedai Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambayo ni taasisi ya kitaifa huru yenye jukumu la kulinda na kuendeleza haki za binadamu, haijachukua hatua stahiki kuhakikisha mtu aliye kwenye ndoa anapata haki ya unyumba na mwenza wake anapohukumiwa kifungo.

Wakili huyo anaiomba Mahakama iamuru walalamikiwa kurekebisha kanuni zinazozuia haki ya unyumba ndani ya kipindi cha miezi miwili iwapo ombi lake litakubaliwa.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa mbele ya majaji Dunstan Ndunguru, Angaza Mwipopo na Mariam Mchomba, Septemba 30, 2025.