Arusha. Wanafunzi 12 wa Shule ya Sekondari Qash, wamepandishwa tena kizimbani Mahakama ya Wilaya Babati, wakikabiliwa na shtaka moja la mauaji ya mwanafunzi mwenzao, Yohana Konki.
Wanafunzi hao waliofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Septemba mosi 2025, leo wamepandishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kesi dhidi yao kutajwa na imepangwa kutajwa tena Septemba 24.
Katika kesi hiyo iliyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Victor Kimario, washtakiwa ni Yason Janes maarufu Bombo, Juma Ally, David Emmanuel, Mahumu Benjamin, Nicolous Apolinary na Benedict Stephano.
Wengine ni Anord Leonard, Laurian Boniphace, Michael Daniel, Nehemia Jeremia, Adam Crispian na Laurent Boniphace.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa la mauaji kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Wakili wa Serikali, Raphael Rwezaula alidai Yason na wenzake 11 walitenda kosa hilo Agosti 16, 2025 katika Kijiji cha Qash, wilayani Babati, mkoani Manyara.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 24, 2025 kwa ajili ya kutajwa kutokana na upelelezi kutokamilika.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mahakamani hapo kesi itasikilizwa kwa njia ya mtandao.
Awali kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, ilidaiwa Yohana alifariki dunia baada ya kupigwa na wanafunzi wenzake kwa madai ya wizi wa kishikwambi, alfajiri ya Agosti 16, 2025 shuleni hapo.
Kamanda alidai uchunguzi wa awali ulionyesha sababu za mauaji hayo ilikuwa mganga wa kienyeji aliyedaiwa kupiga ramli chonganishi. Ilielezwa mganga huyo aliyekimbia na familia yake bada ya tukio hilo alikuwa akiendelea kutafutwa.
Ilidaiwa mmoja wa wanafunzi shuleni hapo aliibiwa kishikwambi, hivyo pamoja na wenzake walikwenda kwa mganga wa kienyeji kupiga ramli kumbaini mwizi, ndipo Yohana (marehemu) akatuhumiwa kwa wizi huo.