Wikiendi kuna vita ya BDL All Star

WACHEZAJI nyota wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), wanatarajia kuonyeshana kazi Septemba 13, kwenye Uwanja wa Donbosco Oysterbay.

Taarifa iliyotolewa na Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD) kupitia Kurugenzi ya Ufundi na Mashindano, imeeleza timu zitaundwa kwa mfumo wa kanda ya Mashariki na kanda ya Magharibi.

Imeeleza pia, makocha watakaosimamia timu hizo upande wa kanda ya Magharibi (West Zone) ni Evarist Mapunda (Pazi) na Barick Kilimba (Stein Warriors).

Kwa upande wa timu ya kanda ya Mashariki (East Zone) ni Mohamed Mbwana (Dar City) na Dauda Maiga (UDSM Outsiders).

Kwa upande wa timu za wanawake, ni Phinius Kahabi (Tausi Royals) na Karim Mbuke (Pazi) watakaosimamia timu ya kanda ya Magharibi (West Zone).

Naye Mohamed Mchenga (DB Lioness) na Maige Yunzu (DB Troncatti) watasimamia timu ya kanda ya Mashariki (East Zone).

Taarifa hiyo imeeleza timu ya kanda ya Mashariki (East Zone) itaundwa na wachezaji nyota kutoka Dar City, JKT, UDSM Outsiders, ABC, Vijana ‘City Bulls’, Chui na Kurasini Heat.

Kwa upande wa kanda ya Magharibi (West Zone), itaundwa na wachezaji nyota kutoka Pazi, Stein Warriors, Savio, Srelio, DB Oratory, Mchenga Star, KIUT na Mgulani Star.

Timu ya wanawake ya kanda ya Mashariki (East Zone), itaundwa na wachezaji nyota kutoka timu za JKT Stars, DB Lioness, DB Troncatti, Pazi Queens, Twalipo Queens, Real Dream, Kurasini Divas na City Queens.

Na timu ya kanda ya Magharibi (West Zone), itaundwa na wachezaji kutoka Jeshi Stars, Tausi Royals, Polisi Stars, Vijana Queens, Ukonga Queens, Kigamboni Queens, Mgulani Stars na UDSM Queens.