NAMBA hazidanganyi. Hata kama ni mechi za kirafiki za kutesti mitambo, lakini kwa nyota wapya sita waliosajiliwa na Yanga msimu huu wote wakiwa wa kigeni ni wazi, wapinzani lazima wajipange kuizuia timu hiyo kutetea mataji, huku kocha wa timu hiyo Romain Folz akichekelea.
Yanga ndio watetezi wa Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA), Kombe la Muungano iliyotwaa yote msimu uliopita.
Hata hivyo, mashabiki wa Yanga wamekuwa na kelele nyingi mitaani kwa sasa wakitambia jeshi lililosajiliwa Jangwani wakiwataka wapinzani wajipange kwa maumivu na hii ikitokana na matokeo ya mechi za kutesti mitambo majembe yao mapya walivyofanya vurugu ya kutupia nyavuni.
Yanga iliyojichimbia kambini Avic Town, Kigamboni kujiandaa na Tamasha la Wiki ya Mwananchi litakalofanyika kesho Ijumaa.
Katika mechi zao tano, Yanga imeshinda zote na kukusanya mabao 15, huku wakiruhusu mara tatu nyavu zao kuguswa, huku nyota wa kigeni wa safu ya mbele wakizalisha mabao 10, matano yakifungwa na wazawa.
Rekodi zinaonyesha katika mabao hayo 15 iliyozalisha Yanga katika mechi zake tano za kirafiki mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Celestin Ecua ndiye kinara akitupia matatu anafuatiwa na Andy Boyeli aliyefungana na Prince Dube na Pacome Zouzoua kila mmoja akifunga mawili, huku Lassine Kouma akitupia moja na kufikia idadi ya mabao 10.
Kwa upande wa wachezaji wazawa Denis Nkane ndiye kinara akiingia kambani mara mbili mabao ambayo ameyafunga kwenye mchezo mmoja mabao mengine mawili yamefungwa na nahodha Bakar Mwamnyeto, Aziz Andabwile na Offen Chikola kila mmoja amefunga bao moja.
Nyota wapya wa Yanga wamezalisha mabao saba, huku nane yaliyosalia yamefungwa na nyota waliokuwapo kikosi tangu msimu uliopita, Pacome mawili sawa na Dube na Nkane, Mwamnyeto na Andambwile wote wakifunga bao moja moja.
Yanga inaendelea kujifua chini ya benchi lake jipya linaloundwa na kocha mkuu, Mfaransa Romain Folz na msaidizi wake Mspaniola Alejandro Manu Rodriguez Lazaro na kocha wa makipa Majdi Mnasria.
Kesho Yanga itashuka tena uwanjani katika pambano la kunogesha Wioki ya Mwananchi kwa kuvaana na Bandari ya Kenya.
Kocha wa Yanga, Folz amesema anafurahishwa na juhudi za wachezaji wa kikosi hicho, huku akiweka wazi, kila mchezaji anaitaka namba kikosi cha kwanza hivyo wamekuwa wakimpa wakati mgumu kutokana na uwezo wanaouonyesha.
“Nimepata bahati ya kukaa na baadhi ya wachezaji kwani wengine bado wapo kwenye majukumu ya timu zao za taifa licha ya kutambulishwa bado sijaona ubora wao lakini kwa waliopo sasa kila mmoja ana nafasi ya kufanya vizuri.
“Juhudi na upambanaji wao unanipa nguvu na naamini nitakuwa na kikosi bora na kipana ambacho kitapambania jezi ya timu hii japo sio rahisi kwangu kusuka kikosi cha kwanza kwani kuna vipaji vingi na kila mchezaji anaitaka namba kikosi cha kwanza.”
Folz akizungumzia utayari wa wachezaji wake kuelekea mechi za ushindani alisema wapo tayari na kwa upande wake pia anaendelea kusuka mbinu mpya kupitia mechi za kimataifa na anavutiwa na namna wachezaji wake wanajituma.
“Nimecheza mechi tano za kirafiki hadi sasa na nimejaribu kutumia kila mchezaji ili kujua ni nani atanipa kitu bora zaidi nafurahia kila mchezaji anataka kuonyesha yeye ni bora na wamekuwa wakifanya hivyo jambo ambalo linanipa imani kubwa ya kuwa na wachezaji wengi bora kikosini ambao wanaweza kunipa matokeo mazuri.”