ZEC yateua 11 kugombea urais, wakabidhiwa magari

Unguja. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imewateua wagombea wote 11 waliorejesha fomu kuwania kiti cha urais Zanzibar.

Pamoja na kuwapa vyeti vya uteuzi, ili kuweka mazingira ya usawa, haki na usalama kwa wagombea wote, wamewapa magari mapya aina ya Toyota Land Cruiser (VXR), mlinzi na dereva.

Akizungumza wakati wa kutangaza uteuzi wao, leo Septemba 11, 2025, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi, amesema hatua hiyo ni kuwasaidia kufanya kampeni zao kwa usalama, uhuru na kuwasaidia kuendesha kampeni kila wanakotaka kufika.

Amesema vyama vilivyochukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania urais vilikuwa 17, lakini vilivyorejesha ni 12.

Hata hivyo, mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Masoud, alishindwa kutimiza vigezo baada ya fomu za wadhamini za mkoa mmoja kutowasilishwa ZEC, hivyo kubakiwa na wagombea 11.

Vyama vilivyoteuliwa ni CCM, ACT-Wazalendo, Makini, ADA Tadea, NCCR-Mageuzi, NRA, ADC, NLD, AAFP, UPDP na TLP.

Kwa mujibu wa Jaji Kazi, gharama zote za kuhudumia magari hayo na kuyafanyia matengenezo zitatolewa na tume mpaka siku ya kutangazwa mshindi wa nafasi hiyo.

“Hatua hii ni kuweka mazingira sawa, salama na amani kwa wagombea. Kwa hiyo, tume imeamua kuwapa magari aina ya VXR ziro kilomita (mapya), mlinzi mmoja, dereva na mafuta. Tume itakuwa inayafanyia service (matengenezo) magari haya kipindi chote cha kampeni,” amesema.

Jaji Kazi amewataka wagombea kufanya kampeni za kistaarabu, kueleza sera zao ili kuendeleza amani na utulivu kwa wananchi.

Kuhusu mgombea wa ACT-Wazalendo ambaye fomu zake zilihitaji uhakiki wa wadhamini, Jaji Kazi amesema baada ya kukamilisha kazi hiyo, ametimiza vigezo na hapakuwa na changamoto nyingine.

Jaji Kazi aliagiza kufanyika uhakiki wa wadhamini wa mgombea huyo, Othman Masoud, baada ya kubainika kutokaguliwa na maofisa wa tume wa wilaya.

Akizungumza wakati wa kutangaza walioteuliwa, Jaji Kazi amesema wamehakiki taarifa hizo na kutimiza vigezo vya mgombea kuwa na wadhamini waliokuwa wanahitajika 200 kila mkoa.

Hata hivyo, amesema wamebaini umuhimu wa kuhakiki wadhamini, kwani hata baada ya kuhakiki waliokuwa wameorodheshwa kumdhamini mgombea huyo, 17 wamebainika hawakuwa na sifa.

“Kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja, jumla ya wanachama 250 waliorodheshwa kuwa wadhamini. Hata hivyo, katika uthibitisho uliofanywa, jumla ya wanachama 11 waligundulika taarifa zao hazikuwa sahihi kwa vile namba za kadi za wanachama hao hazikuendana na majina yao,” amesema na kuongeza:

“Kwa Mkoa wa Kusini Unguja, jumla ya wanachama 207 waliorodheshwa kuwa wadhamini. Hata hivyo, katika uthibitisho huo, wanachama sita waligundulika taarifa zao hazikuwa sahihi kwa vile namba za kadi za wanachama hazikuendana na majina.”

Wakizungumza baada ya kuteuliwa na kukabidhiwa magari, baadhi ya wagombea wameishukuru tume kwa kuweka mazingira wezeshi, kwani katika kipindi cha nyuma walikuwa wakishindwa kuendesha kampeni zao kwa kukosa usafiri.

Mgombea wa ADA Tadea, Juma Ali Khatib amesema: “Wakati mwingine mtu alikuwa akitumia baiskeli au pikipiki kufanya kampeni, kwa kweli mazingira yalikuwa magumu.”

Mgombea wa NCCR-Mageuzi, Laila Rajab Khamis, amesema hatua hiyo ni kuwasaidia zaidi wanawake ambao mara nyingi wamekuwa wakikabiliwa na vikwazo vya ukata.

“Haya ni mazingira rafiki kwa kila mgombea, tunashukuru na tunaahidi kufanya kampeni za kistaarabu kuhakikisha amani na usalama unadumishwa,” amesema.