Morogoro. Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro iliyoketi wilayani Kilombero imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa mshtakiwa Elopi Kibolile (33) baada ya kupatikana na hatia kwa kosa la kumuua binti wa miaka 14 mwanafunzi wa shule ya msingi (jina limehifadhiwa) iliyopo kata ya Mchombe, halmashauri ya Mlimba Wilaya ya Kilombero.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji wa Mahakama Kuu, Stephen Magoiga baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ambao haukuacha shaka katika kuthibitisha shtaka lililokuwa likimkabili mshtakiwa huyo ambaye ni mkazi wa Mchombe.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa ukisimamiwa na wakili Dastan William na Emanuel Kahigi ambapo imedaiwa kuwa mshtakiwa huyo ametenda kosa hilo Aprili 29, 2024 ambapo kabla ya kumuua mwanafunzi huyo, aliyekuwa alitokea shule alimbaka, kumuua kisha mwili wake kuutupa porini.
Akisoma maelezo ya shitaka kabla ya hukumu hiyo wakili Dastan William amesema baada ya mshtakiwa kufikishwa mahakamani upande wa Jamhuri ulipeleka mashahidi 15 akiwemo daktari, mkemia wa Serikali pamoja na dada wa marehemu ambao kwa pamoja walitoa ushahidi ambao Mahakama iliridhishwa nao na kumtia hatiani.
Baada ya hukumu wakili wa upande wa utetezi, Funuki Sikujua ameeleza kuwa kwa sasa anasubiri maamuzi ya mshtakiwa ama ndugu wa mshtakiwa, kama wataamua kukata rufaa ama kutokata rufaa.
Akitoa maoni yake kufuatia hukumu hiyo, Wakili Sikujua ameeleza kuwa Mahakama imetoa hukumu kwa kuzingatia maamuzi ya mshtakiwa aliyoyachagua ya kukaa kimya wakati alipopewa nafasi ya kujitetea.
“Uendeshaji wa kesi ya jinai una hatua mbalimbali mojawapo ni ya utetezi na hii inakuja baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao na Mahakama inapoona mshatakiwa anayo kesi ya kujibu, ambapo hutoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea.
Sheria inaelekeza mshtakiwa anaweza kujitetea kwa kiapo au bila ya kiapo au kuamua kukaa kimya, haya yote mteja wangu nilimweleza lakini yeye alichagua kukaa kimya,” ameeleza wakili Sikujua.
Ameongeza, “Baada ya kuchagua kukaa kimya akimaanisha kuwa anaiachia Mahakama nilikaa na mteja wangu na nikamweleza madhara ya kukaa kimya lakini bado aliendelea kushikilia msimamo wake wa kukaa kimya, hivyo hukumu hii iliyotolewa siwezi kuiongelea chochote kwani imetolewa kwa kuzingatia maamuzi ya mshtakiwa mwenyewe, kwa msingi huu siwezi kusema kuwa hukumu iko sawa ama haiko sawa.”
Amesema baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, amezungumza na mteja wake ambaye ameonesha nia ya kukata rufaa, hata hivyo mpaka sasa bado hajapata taarifa za mshtakiwa huyo wala ndugu zake kama wameanza taratibu kutimiza azma hiyo.