Bado Watatu – 26 | Mwanaspoti

NILIPOWAZA hivyo, nilipunguza mwendo zaidi, nikawa natupa macho huku na huku. Nikaona kulikuwa na pikipiki nyuma yangu. Niliona jamaa amempakiza mwenzake. Aliyempakia mwenzake alikuwa mwanaume, lakini sikuweza kuona aliyepakiwa alikuwa mwanaume au mwanamke. Nilitaka ile pikipiki inipite lakini ilikuwa ikienda mwendo wa taratibu.

Nikakata kushoto ambako kulikuwa na barabara ya mchanga. Sasa makaburi yalikuwa kulia kwangu. Sikushughulika tena na ile pikipiki, nikasimamisha gari.

Baada ya kuwaza kwa sekunde kadhaa, nikaona niingize lile gari ndani kabisa ya makaburi ili niweze kuitoa ile maiti na kuitupa. Nikaliingiza gari hilo na kulisimamisha chini ya mti wa mwembe.

Nikafungua mlango na kushuka. Nikatazama kila upande. Nilipoona kulikuwa na kiza, nikafungua mlango wa nyuma. Mwili wangu ulikuwa ukisisimka, lakini nilijikaza kwa vile nilijua nisipojikaza maisha yangu yameshaharibika.

Baada ya mlango wa gari kufunguka, niliishika miguu ya Shefa nikaivuta kwa nguvu nje ya gari. Mwili wa Shefa uliburuzika, ukatoka kwenye gari na kuanguka chini.

Wakati nafanya hivyo, niliona mwanga wa kitochi cha simu ukiumulika mwili huo. Nikashituka. Mwanga huo ulitokea nyuma ya ule mti wa mwembe uliokuwa karibu yangu. Nikahisi kulikuwa na mtu aliyekuwa amejificha akinimulika. Sikujua mtu huyo alikuwa nani. Kile kitendo cha kugundua kuwa kuna mtu alikuwa akiniona kilichafua akili yangu, nikafunga mlango wa gari na kukimbilia kwenye mlango wa dereva ambao nilikuwa nimeuacha wazi. Nikajipakia kwenye gari haraka haraka.

Yule mtu aliyekuwa akinimulika kitochi akajitokeza. Kwa sababu ya ule mwanga kuelekea kwangu sikuweza kumuona. Sikujua alikuwa mwanaume au mwanamke ila nilisikia viatu vyake. Alikuwa akinikimbilia, labda alitaka aniulize nimeacha nini.

Nikaliwasha gari haraka na kulirudisha kinyume nyume. Kama nisingekuwa makini ningeikanyaga ile maiti niliyoitupa. Tairi zilipita sentimita chache tu mbele ya kichwa cha Shefa!

Nilipolitoa gari katika eneo hilo nikaiona ile pikipiki iliyokuwa nyuma ya gari langu wakati nafika pale. Ilikuwa imeegeshwa pembeni mwa barabara na kijana mmoja alikuwa amekaa juu yake kama vile alikuwa akisubiri mtu.

Nikajiuliza yule mtu aliyekuwa amempakia yuko wapi na pale alikuwa akisubiri nini?

Nilimuangalia kwa makini kijana huyo lakini sura yake ilikuwa ngeni machoni mwangu. Nikatia gia ya kwenda mbele na kuondoka kwa kasi mahali hapo.

Tayari kile kitendo cha kuwaona wale watu kilikuwa kimeshanitia wasiwasi. Wakati naendesha, kila mara nilikuwa ninatazama nyuma kuiangalia ile pikipiki lakini sikuiona tena.

Nikafika nyumbani kwangu salama. Nilifungua geti, nikaliingiza gari kisha nikaenda kuoga.

Nilipotoka bafuni nikakaa kitandani na kujiuliza tena, yule aliyenimulika kitochi alikuwa nani? Alikuwa akinichunguza mimi au alikuwa na hamsini zake?

Na yule aliyekuwa na pikipiki, alikuwa ni mwenzake? Au naye alikuwa na hamsini zake?

Haikuwa rahisi kupata jibu la uhakika zaidi ya kukisia tu. Wapo watu wanaokwenda makaburini usiku kuzika makafara yao, inawezekana tumekutana kwa bahati mbaya, nikajiambia.

Nikawaza pengine yule mtu niliyemuona amepakiwa kwenye pikipiki alikuwa akipelekwa huko huko makaburini nilikokuwa ninakwenda mimi kwa shida hizo za kichawi.

Licha ya kujaribu kujipa moyo kuwa watu wale walikuwa hawanijui, bado nilipata wasiwasi. Nilikosa amani na usiku ule sikupata usingizi kabisa.

Nilijiambia hata kama walikuwa watu ambao hawanijui, watakapoiona ile maiti niliyoitupa wanaweza kwenda kutoa ripoti polisi. Kituo cha polisi cha Mabawa hakikuwa mbali sana na eneo lile.

Polisi wakiambiwa kuna gari lililoacha maiti na kukimbia, watakwenda makaburini hapo. Watakapogundua kuwa maiti hiyo ni ya mtu anayetafutwa, watataka kujua aina ya gari na namba ya usajili ya gari hilo lililoipeleka maiti huyo.

Kama wale watu wamezisoma namba za usajili za gari langu, ndio nimekwisha!

Usiku huo sikupata usingizi hata chembe kwa mawazo. Hisia zangu zilikuwa kwenye kukamatwa tu. Ile hofu niliyokuwa nayo ilinitengenezea picha akilini mwangu nikamuona yule mtu aliyenimulika kitochi akienda kuripoti polisi.

Polisi wanafika katika lile eneo na kuiona maiti ya Shefa.

Wanamuuliza yule mtu kama ameiona namba ya usajili ya gari langu. Yule mtu anawajibu kuwa ameiona na anawatajia.

Hata sikuweza kuwaza jinsi polisi hao walivyonitambua isipokuwa picha ya polisi wakiwasili nyumbani kwangu ikanijia akilini. Nikawa najigutuka kila niliposikia sauti ya viatu barazani au sauti ya kuguswa kwa mlango.

Nilipata usingizi kidogo tu wakati wa alfajiri. Kile nilichokuwa ninakiwaza nikakiota. Niliota polisi wamefika nyumbani kwangu. Mlango waliukuta wazi, wakaingia ndani.

“Wewe ndiye uliyekwenda kutupa maiti kule makaburini?” Polisi mmoja akaniuliza.

Kabla sijajibu, polisi mwingine akaingilia kati.

“Ndiye huyo huyo, unaona anavyohema kwa hofu.”

“Sio mimi. Sijakwenda kutupa maiti,” nikajitetea ili nisikamatwe.

“Wewe mwanamke mwongo sana, umeua mtu kisha umekwenda kumtupa halafu unakataa. Hebu tueleze yule mtu amekukosea nini?”

“Mke wake anamtafuta tangu juzi, kumbe umemuua!” Polisi mwingine akanishangaa.

Nikaona ninakamatwa na kupelekwa kituo cha polisi. Hapo hapo nikashituka. Moyo ulikuwa ukinienda mbio na sikutaka kulala tena. Hata hivyo usingizi ukanipitia tena.

Safari hii nikaota niko mahakamani nimeshitakiwa kwa kosa la kumuua Shefa. Mume wangu, mke wa Shefa pamoja na Raisa walikuwa mahakamani wakinitazama.

“Upande wa mashitaka umethibitisha bila shaka yoyote kwamba wewe umemuua mume wa mwenzako kwa sababu ya kumuonea wivu mwenzako. Kwa hiyo mahakama hii inakuhukumu…”

Kabla ya jaji kumaliza kunisomea hukumu yake, nilipiga ukelele ulioniamsha usingizini. Nilipozinduka niliona mwili wangu umetota jasho na moyo wangu ukiendelea kunienda mbio.

Safari hii niliinuka na kutoka sebuleni. Nikawasha taa na kukaa kwenye kochi. Kama shetani ameamua kunichezea, basi sitalala tena, nikajiambia kwa hasira.

Kweli nilikaa hapo hadi asubuhi. Nilipoona kumekucha nilijishauri niingie chumbani nilale tena lakini niliogopa kwa kuhisi kuwa nitaendelea kuota ndoto za kunitisha.

Kule kukosa usingizi kuliufanya mwili wangu uchoke na uso wangu ulikuwa kama wa mgonjwa wa homa.

Nikaenda bafuni kuoga. Nilipotoka bafuni nilivaa nguo na kurudi tena sebuleni kusubiri saa mbili ili nitoke niende saluni.

Ghafla mume wangu akanipigia simu.

“Habari ya asubuhi,” akanisalimia baada ya kupokea simu yake.

“Nzuri. Unapiga kutoka wapi?” nikamuuliza.

“Tuko mpakani Tunduma, hatujavuka bado. Hili eneo lina mbu wengi. Tangu jana najisikia kuumwa, nahisi nimepata malaria.”

“Kama hali itazidi kuwa mbaya nitampigia meneja wetu nimuarifu ili alete dereva mwingine. Mimi naweza kurudi.”

“Utarudi huku Tanga?”

“Kwanza nitakwenda hospitali kisha nitakuja huko kama nitapewa ruhusa.”

Nikanyamaza kidogo kabla ya kumjibu.

“Basi utanijulisha kila litakalotokea.”

“Mke wa Shefa aliwahi kunipigia kumuulizia mume wake. Vipi amesharudi?”

“Sijajua kama amerudi,” nikamjibu.

“Namjua Shefa, yule ni mtu wa wanawake. Si ajabu amejichimbia na mwanamke gesti, amemsahau hata mke wake!”

Alikuwa amepatia kidogo kwani hata kama Shefa ameuawa lakini aliuawa akiwa kwa mwanamke na mwanamke mwenyewe ni mimi, nikajiambia kimoyomoyo.

Kwa kweli nilijuta kutembea na yule kaka!

Nilikuwa na mengi ya kumueleza Sufiani likiwamo suala la lori la Shefa kupinduka na kumuua dereva wake, lakini sikutaka kumwambia lolote.

Sufiani akaniaga na kukata simu.

Nikasikia mlango unabishwa. Moyo ukanilipuka tena. Nikainuka na kwenda kuufungua. Nikamuona Raisa kwenye mlango.

“Karibu. Habari ya huko,” nikamwambia huku nikimpisha kwenye mlango.

Nilihisi kuwa Raisa alikuwa amekuja na jambo. Asingekuja kwangu asubuhi ile.

“Vipi shoga?” nikamuuliza tulipoketi kwenye makochi.

“Shoga, nilikuona jana usiku kule makaburini!”

Mwili wangu uliishiwa na nguvu ghafla. Nikahisi kama vile moyo wangu ulikuwa umesimama! Nikabaki nimeduwaa. Raisa akaendelea kuniambia.

“Mwenzako jana sikupata usingizi kwa kukufikiria wewe. Nilishindwa hata kukupigia simu kukuuliza,” Raisa akaniambia.

“Kwani kumetokea nini shoga?”

“Kuna tukio nimeliona na limenitatanisha sana, sasa sijui ulikuwa ni wewe au siye?”

“Tukio gani, hebu nidokeze?”


“Jana usiku nilikwenda klabu, nikarudi majira ya saa saba hivi. Wakati nipo kwenye bodaboda nikaliona gari lako linaelekea kule Msambweni makaburini. Nikamwambia bodaboda alifuate…”

“Gari langu mimi?” nikamuuliza ghafla baada ya maelezo yake kuanza kunishitua.

Moyo wangu ulipiga kwa kishindo. Mwili wangu ukaishiwa na nguvu ghafla.

“Niliona gari lako, si nalijua…”

“Uliliona linakwenda makaburini…?” nikajidai kumuuliza kwa mshangao wakati anaendelea kunieleza. Nilimkatiza kusudi kwa sababu nilishajua alitaka kunieleza nini.

Itakuwa yeye ndiye aliyekuwa amepakiwa kwenye ile pikipiki niliyoiona usiku uliopita kule makaburini na bila shaka ndiye aliyenimulika na kitochi cha simu wakati nautupa mwili wa Shefa!

Kama ni hivyo, nilijiambia kimoyomoyo, kila kitu kimeshafahamika. Balaa gani hili jamani! Nikalaani.

“Mimi nikalifuata hilo gari hadi makaburini. Nikaona linaingia ndani. Nikashuka kwenye bodaboda kukufuata ili nikuulize kulikoni. Kwanza sikuwa na uhakika kama ni wewe ulikuwa ukiendesha, nikajificha kwenye mti kuchungulia nikakuona unashuka kwenye gari na kushusha kitu ukakitupa chini…”

Vile Raisa alinieleza moyo wangu ulikuwa unakwenda kasi kama saa! Nilikuwa nimemtolea macho nikimsikiliza. Sikuwa hata na la kupinga kwani ukweli ukidhihiri uongo hujitenga.

Raisa alipoona nipo kimya aliendelea kuniambia.

“Sasa mwenzangu nawasha kitochi ili nione kama ni wewe, ukakurupuka na kuingia kwenye gari, ukarudi nyuma na kuondoka. Haya niambie ulikwenda kutupa nini usiku ule? Hata huogopi!”

Kumbe hukuona nilichokitupa au unaniuliza tu usikie nitasema nini? Nikajisemea kimoyomoyo.

Kwanza nilijidai kuguna kama vile hilo jambo alilonieleza nilikuwa silijui. Nilishajua kuwa iwapo nitajiingiza kusema nilikuwa ni mimi, moja kwa moja nitahusika na kifo cha Shefa. Na nitaonekana nilimuua mimi kisha nikaenda kumtupa makaburini.

“Mbona shoga jana sijatoka. Nilikuwa hapa nyumbani,” nikamwambia huku nikijaribu kuifanya sauti yangu kuwa tulivu isiyo na taharuki.

“Hujatoka! Mbona niliona mtu kama wewe?”

“Siye mimi. Binadamu tunafanana tu.”

“Kwani kuna mtu ulimuazima gari lako jana?”

Nilitaka nikubali kuwa nilimuazima mtu lakini nilijiuliza, nitakapokuja kuulizwa nilimuazima nani nitajibu nini? Nikaona nikatae.

“Sijamwazima mtu. Hilo gari naliendesha mwenyewe tu na tangu jana sijatoka nalo. Nitoke niende wapi shoga?”

“Mmh…! Basi mimi nilidhani ni wewe ndio maana nilikufuata. Kumbe siye!”

“Hicho kitu alichokitupa huyo mtu kilikuwa kitu gani?” nikamuuliza ili nijue kama ameugundua mwili wa Shefa.

“Sijakiona. Mahali penyewe palikuwa na giza. Nilipoona mtu mwenyewe anakimbia na mimi nikaondoka. Nafikiri bodaboda wangu alizosoma namba za lile gari, nitakwenda kumuuliza.”

“Si uliache tu shoga. Pengine mtu amekwenda kutupa makafara yake makaburini, utajuaje?”

“Inawezekana. Hata mimi kuna siku niliambiwa na mganga nikazike kitu kwenye kaburi nikashindwa.”

Nikajidai kucheka lakini sikuweza. Uso wangu ulikuwa umekakamaa na haukutaka kukunjuka kutokana na hofu na fadhaa niliyokuwa nayo.