BURUDANI mbalimbali za muziki ukiwemo wa Bongofleva zimeendelea kuteka hisia za mashabiki wa soka waliojitokeza katika kilele cha Wiki ya Mwananchi kinachofanyika leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ndani ya uwanja huo mashabiki waliojitokeza wamekuwa wakiburudishwa na nyimbo mbalimbali huku wakiwa katika furaha wakati tamasha hilo likiendelea kushika kasi.
Wakati hali ya mashabiki ndani ya uwanja inaendelea kuongezeka kadri muda unavyosonga mbele nyuso zenye furaha zinaendelea kuonekana kutokana na burudani maridhawa iliyopo.
Tamasha la leo litasindikizwa na mechi ya kimataifa ya kirafiki kati ya Yanga dhidi ya Bandari kutoka Kenya.
Tamasha hilo linaendelea kukua na kuteka hisia ya mashabiki wa kikosi hicho tangu lilipoasisiwa mwaka 2019 chini ya uongozi wa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msolla.