Dk Biteko: Hakuna matokeo bila tathmini

Mwanza. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amezitaka taasisi za umma na binafsi kuhakikisha zinafanya ufuatiliaji na tathmini ya mara kwa mara ili kujiandaa na athari zinazoweza kujitokeza, kwa kuwa tayari zitakuwa na suluhu mkononi.

Amesema mtu au taasisi isiyofanya tathmini hujikuta ikishangazwa na matokeo badala ya kuyatabiri na kujiandaa mapema.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Septemba 12, 2025 jijini Mwanza, alipofunga kongamano la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

“Mtu anayefanya tathmini na ufuatiliaji, hata madhara yakitokea yatakuwa madogo kwa sababu tayari ameona changamoto mapema na ameshaandaa majibu mkononi,” amesema na kuongeza:

“Serikalini lazima tuchukue mfumo wa kufanya tathmini, tena bila kuhurumiana. Hatuwezi kuridhika na kusikia habari njema pekee, bali ukweli ndiyo msingi wa hatua za maendeleo.”

Amesema washiriki wa kongamano hilo ni kama waamuzi wa mchezo wa mpira wa miguu, akiwataka waendelee kuwa waadilifu, kuonyesha upungufu bila woga na kutangaza mazuri kwa sauti kubwa ili wananchi waone thamani ya Serikali yao.

Dk Biteko amesema tathmini iliyofanyika imeonyesha asilimia 40 ya washiriki bado wako katika hatua za awali za kujifunza namna ya kuandaa viashiria vya ufuatiliaji na tathmini, huku asilimia 50 wakibainika hawana kabisa ujuzi wa kuandaa KPI (kigezo cha ufanisi wa utendaji).

“Hii ni kioo chetu. Miaka miwili ya makongamano haya tumefikia asilimia 50, sijajua mwakani tutakuwa na hali gani. Sasa ninyi wataalamu ndio tunawaamini mtusaidie,” amesema.

Amewataka kuonyesha udhaifu bila kumuogopa mtu, akiwakumbusha kuelezea umma programu na miradi inayotekelezwa na Serikali kwa wananchi.

Dk Biteko amesema hatua za kuweka mfumo wa tathmini endelevu zinasaidia kupunguza makosa na kuhakikisha kila sekta inatoa huduma bora kwa wananchi.

“Mtu yeyote anayejaribu kukurudisha nyuma katika kazi ya tathmini anajua anachokifanya. Huu ni wajibu wetu na hatuwezi kurudi nyuma. Tunataka wananchi wajue kuwa Serikali yao inafanya kazi kwa uwazi na kwa usahihi,” amesema.

Dk Biteko amesema ni muhimu kuwa na mpango mkakati wa tathmini kwa kila wizara, idara na taasisi ili kuhakikisha maendeleo ya nchi hayazuiliwi na changamoto zisizotarajiwa.

Awali, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Stanslaus Nyongo amesema kujitathmini ni msingi wa maisha na maendeleo endelevu.

“Ufuatiliaji ndiyo njia pekee ya kubaini ufa kabla haujawa ukuta. Ni kweli ni gharama, lakini kutokufanya tathmini na ufuatiliaji ni gharama kubwa zaidi kwa taasisi na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Amesema ufuatiliaji na tathmini pia unasaidia kubaini changamoto za kiutendaji mapema, kufanya marekebisho na kuongeza uwajibikaji kwa watendaji wa sekta zote.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk James Kilabuko akimwakilisha Katibu Mkuu, Dk Jim Yonaz amesema kongamano hilo limekuwa jukwaa la kipekee la kubadilishana uzoefu kati ya washiriki kutoka Serikali Kuu, mamlaka za mitaa, taasisi binafsi, mashirika ya kimataifa na wataalamu wa ndani na nje ya nchi.

“Kwetu tunaona haya kama mafanikio ya kipekee ya kuongeza ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika eneo la ufuatiliaji na tathmini,” amesema.

Kongamano hilo limehusisha wataalamu kutoka Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Cameroon, Ghana, Ujerumani, Zambia na Zimbabwe. Washiriki wamejifunza kupitia mada mbalimbali, mijadala ya kitaalamu, mafunzo na maonyesho.